Kuwa na mahusiano ya kimapenzi na mfanyakazi mwenzako si jambo linalokatazwa moja kwa moja. Ingawa kuna baadhi ya kampuni sheria zao haziruhusu kwa sababu maalumu.
Kabla haujaanza mahusiani na mfanyakazi mwenzako zingatia mambo haya.
Angalia sera za kampuni
Kila sehemu ina sera zake kuhusu mahusiano baina ya wafanyakazi. Baadhi ya sehemu huruhusu mahusiano ya kimapenzi kati ya wafanyakazi kikubwa yasiharibu utendaji kazi.
Licha ya hivyo kwenye ofisi nyingine sera zinakataza kabisa kutokana na hatari zinazoweza kutokea.
Kama mmoja wenu ni bosi wa mwingine uhusiano wa kimapenzi unaweza kuwa hatari zaidi. Hii inaweza kusababisha upendeleo wa wazi au wa kufikiriwa na wafanyakazi wengine.
Pia migongano ya kimaslahi, hasa wakati wa kufanya maamuzi ya kiutendaji kama vile kupandisha cheo au kutoa adhabu, inaweza kusababisha matatizo ya kisheria, hasa kama mmoja wenu atahisi baadaye kuwa alilazimishwa au kubanwa kihisia.
Fikiri kuhusu mahusiano yatakapovunjika, mahusiano yoyote huwa na uwezekano wa kuvunjika. Je, unaweza kufanya kazi kwa karibu na mtu huyo kila siku endapo mambo yataharibika? Hilo ni swali unapaswa kujiuliza kabla ya kuingia naye kwenye mahusiano.
Ikiwa utachagua kuendelea na uhusiano huo, hakikisha mnafanya kila jitihada kudumisha uweledi (professionalism) na usilete mapenzi kazini jitahidi kutenganisha maisha binafsi na kazi, weka mipaka iliyo wazi, hasa kama mnafanya kazi pamoja kwenye timu moja.
Linganisha hatari na faida, mahusiano ya kazini yanaweza kufanikiwa sana kuna wapenzi wengi waliokutana kazini na kuoa. Lakini pia kuna waliopoteza kazi au sifa kwa kushindwa kuweka mipaka.
Hivyo jiulize maswali haya kabla ya kuingia kwenye uhusiano. Je tunafanya kazi kwenye idara moja? Je, mmoja wetu anamwajibisha mwingine moja kwa moja? Je, tunajua madhara yanayoweza kutokea kazini? Je, tutadumisha heshima na weledi ikiwa uhusiano hautadumu?.
Si vibaya kuwa na mahusiano ya kimapenzi na mfanyakazi mwenzako, lakini inahitaji tahadhari kubwa, uelewa wa sera za kampuni au sehemu unayofanyia kazi.
Leave a Reply