Mwanamuziki wa Bongo Fleva na CEO wa Next Level Music, Rayvanny ameweka wazi kuwa wakati Mbosso amepanga kuondoka WCB alimfuata na kumuomba ushauri.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, leo Machi 19,2024 Vanny Boy amesema alimtaka Mbosso kusonga mbele bila kusikiliza maneno ya watu
“Nilimwambia wale wale wanaokusifia ndio watakaokuponda. Bahati Bukuku alisema ‘unapoianza safari wanakutia moyo, unaoonyesha mafanikio vinaibuka vikwazo’ kwahiyo unapoona unatukanwa sana you have to know kwamba wewe ni mti wenye matunda na umekuwa unatakiwa uweke nguvu uendelee kusonga mbele.
“Ofcouse aliniuliza tuliongea tukashauriana nashukuru uongozi pia wa WCB wameweza kumuachia bila complication zozote. Ameachiwa huru kuendelea kufanya kazi zake,” amesema Vanny Boy
Akizungumza kuhusu uamuzi wa msanii kuondoka kwenye lebo ameweka wazi wengi wanaondoka kwa ajili ya kukua na kuongeza ujuzi.
“Ukizungumzia Mbosso ni msanii ambaye anapendwa na watu wengi sana, watu wanapenda uwezo wake, msanii ambaye anaonesha uwezo muda mrefu. Mimi nitazungumzia msanii kutoka kwenye lebo ni kwamba anakuwa anataka confort zone ya kufanya vitu vyake ambavyo anaamini yeye viko sawa.
"Kitu kingine ni ukubwa wa msanii kwamba nataka nikue sasa nitoke nyumbani huwezi ukawa wewe miaka yote uko nyumbani tu. Inabidi utoke kesho usikie Mbosso naye ana ‘Khani FC’ au ana lebo yake inayowasaidia watu wengi,” ameeleza Rayvanny
Utakumbuka mapema Machi Rayvanny aliweka wazi mbinu aliyotumia kuondoka WCB akieleza kuwa kabla ya kutaka kujiondoka Wasafi alikutana na Wizkid Zanzibar ambapo nyota huyo wa Nigeria alimshauri.
Rayvanny alijiunga na WCB mwaka 2015, akiwa ni msanii wa pili, baada ya miaka sita ya kufanya kazi pamoja, aliachana nao akiwa tayari amefungua lebo yake, iitwayo ‘Next Level Music (NLM)’ ambayo inamsimamia msanii Mac Voice.
Kwa sasa WCB imebakiwa na wasanii watatu baada ya Mbosso kujikataa wasanii hao ni Zuchu, Lava Lava na D Voice huku kukiwa na tetesi za kuingiza wasanii wapya.

Leave a Reply