Peter Akaro
Alianza mapambano yake katika sanaa akiwa tayari ni mama wa watoto wawili, ni wachache walioamini Shilole atakuja kuwa chapa kubwa hivi, safari ilianza polepole kama haendi ila sasa ameenda hata kule ambako hakutarajiwa.
Kwa bahati mbaya hajawahi kutajwa katika orodha ya wanamuziki au waigizaji wakali ila ni sasa ni mmoja ya watu waliofanikiwa na wenye ushawishi katika tasnia ya burudani nchini.
Jina la Shilole alipatiwa na bibi yake na maana ya jina hilo katika kabila la wanyamwezi ni kioo, hiyo ni kutokana alipokuwa mdogo wakati akilia bibi yake alikuwa akipatia kioo, na pindi alipojiangalia, basi mara moja alinyamaza.
Katika safari yake ya muziki Shilole kamwe hawezi kumsahau Q Chief kwa sababu ndiye aliyempeleka studio kwa C9 ambapo alilipa Sh300,000 kwa ajili ya kurekodi, hilo limefanya wawili hao kuwa na ukaribu mkubwa hadi sasa.
Hata hivyo, kabla ya kutambulika ndani ya Bongofleva, Shilole alikuwa ni muigizaji, filamu ya kwanza kucheza inaitwa 'First Decision' ambayo alishirikiana na majina makubwa katika tasnia hiyo kama Ray Kigosi na Irene Uwoya.
Shilole ni staa mwingine aliyeanzia upande wa filamu kisha kuja kutengeneza himaya yake katika Bongofleva, wengine ni Snura, Queen Malaika, Lulu Diva, Hamisa Mobetto n.k.
Nyimbo za mwanzo zilizompa umaarufu Shilole ni kama Nakomaa na Jiji (2013), Paka la Baa (2013) ft. Hasani Vocha, Namchukua (2013), Chuna Buzi (2014), Malele (2014), Nyang'anyang'a (2015) na Say My Name (2016) ft. Barnaba.
Video ya wimbo wake 'Say My Name' ulioandikwa na Barnaba ilishika namba moja katika chati za Soundcity nchini Nigeria, huku video ya wimbo 'Malele' ikiwa ya kwanza kwake kufanyika katika nchi tatu tofauti ambazo ni Tanzania, Uholanzi na Ubelgiji.
Kabla ya kuishika Bongofleva Shilole alionekana katika video ya wimbo wa 20 Percent, Tamaa Mbaya (2011) na baada ya kutoka kimuziki akaonekana katika video ya wimbo wa Nuh Mziwanda, Msondo Ngoma (2014) na ile ya Rayvanny, Natafuta Kiki (2016).
Mwaka 2016 alifungua rekodi lebo yake ya kwanza, Shilole Entertainment na kumsaini Amaselly, ingawa msanii huyo hakufika mbali kimuziki haikuwa sababu ya Shilole kuachana na mpango huo moja kwa moja.
Akaja kufungua lebo nyingine, Shishi Gang (2020) na punde akamsaini Ronze ambaye tayari alikuwa amefanya kolabo na wasanii kama Amber Lulu na Mr. Blue.
Hata hivyo, Ronze hakuwa na maisha marefu ndani ya Shishi Gang akajitoa, Desemba 2023 Shilole akamsaini msanii mwingine, Nice ambaye alitoka na wimbo unaokwenda kwa jina la Fora.
Shilole ni miongoni mwa wasanii wa mwanzo wa kike Bongo kufungua lebo, wengine ni Shaa (SK Music), Vanessa Mdee (Mdee Music), Nandy (The African Princess Label), Hamisa Mobetto (Mobetto Music) n.k.
Kipindi ana uhusiano na Nuh Mziwanda waliunda kundi lao 'Shiwonder' ikiwa ni muunganiko wa majina yao, waliotoa wimbo mmoja tu, Ganda la Ndizi (2015) ambao ulikuja baada ya kuwepo tuhuma za kuwa Nuh analelewa na Shilole kitu kinachopelea kuvumilia vipigo.
Na hadi sasa bado Shilole hajatoa albamu wale EP, huku akiwa amechaguliwa zaidi ya mara tatu kuwania tuzo za muziki Tanzania (TMA) bila ushindi wowote.
Licha ya hilo, Shilole ni msanii wa pili wa kike wa Bongofleva mwenye wafuasi (followers) wengi katika mtandao wa Instagram, kwa ujumla ametanguliwa na Diamond Platnumz na Hamisa Mobetto pekee.
Kwa Afrika Mashariki Shilole ni mwanamke wa tano kuwa na wafuasi wengi Instagram baada ya Zari The Bosslady (Uganda), Hamisa Mobetto (Tanzania), Wema Sepetu (Tanzania) na Lupita Nyong'o (Kenya).
Wengi wanajiuliza ilikuwaje ghafla Shilole akapata wafuasi wengi hivyo, ukweli ukiachana na muziki na biashara zake, usheshi wake katika mitandao, mahojiano na vyombo vya habari na matukio mengine vimempa mashabiki wengi.
Ikumbukwe Selena Gomez ndiye mwanamuziki mwenye wafuasi wengi Instagram duniani akiwa nao milioni 421, huku Influencer Marketing Hub wakimtaja kulipwa Dola2.5 milioni ili kushapisha tangazo moja katika ukurasa wake.
Kutokana na ushawishi wake katika mitandao, Shilole ni miongoni mastaa Bongo wenye dili nyingi za ubalozi, kila mara ya anasaini mikataba mipya, chapa mbalimbali zinahitaji kufanya naye kazi.
Shilole ambaye amewahi kuwa miongoni mwa Majaji wa Bongo Star Search (BSS), ana ushawishi na amekuwa akichukua dili nyingi kuliko baadhi ya wasanii wengi ambao kazi zao zinafanya vizuri katika tasnia kwa sasa, huyu ndiye Shilole a.k.a Shishi Baby, kama haendi ila ndio anaenda hivyo!.
Na hilo limefanya biashara yake ya chakula, Shishi Food kuzidi kufanya vizuri sokoni na hata kuwavutia mastaa wengine Bongo kama Idris Sultan, Lamar, Isha Mashauzi nao kufanya biashara hiyo. Tayari Shilole amejenga nyumba yake iliyogharamu zaidi ya Sh90.

Leave a Reply