Wasanii wa hip hop wanajua  kuchambua mambo, lakini..

Wasanii wa hip hop wanajua  kuchambua mambo, lakini..

Kelvin Kagambo


Sina lengo la kumshushia mtu heshima ukweli mchungu ni lazima usemwe. Wasanii wa hip hop wa Tanzania ni vichwa kuliko wanaofanya muziki wa kuimba a.k.a wasanii wa Bongofleva kama tulivyozowea kuwaita.

Kama huamini fuatilia inapotokea mijadala inayohusisha wasanii katika kutoa hoja wale wa hip hop huzungumza vitu konki sio poa. Unasikiliza msanii anatema hoja za moto mpaka unatingisha kichwa unasema Yes! Hapa kuna mtu mzima mwenye akili timamu anazungumza. 

Wanajua kuchambua mambo, ni wazungumzaji wazuri, wanajua kupangilia maneno, wanajua kuelezea na kujielezea, wanajiamini, wameelimika, wengi wamesoma mpaka levo za juu za elimu na vitu vyote hivyo vinawafanya waonekane wana akili sana. 

Na ndiyo maana wala haishangazi kuwaona kina Sugu, Profesa Jay, Mwana FA wamejazana bungeni na sio kwa ajili ya kupiga meza tu, bali kuchangia hoja.

Lakini wanapoongea wasanii wa Bongofleva kwanza kuwa makini sana. Kama unatumia simu hakikisha umevaa ‘earphone’ wenyewe hawajali. Wanaweza kuzungumza neno lolote bila kujali. Ni wachache sana kukuta wasanii wa Bongofleva wanaongea vitu vya maana. Wengi hawajui vitu vingi hata vinavyohusiana na tasnia yao. 

Sikiliza hata muziki wale wa hip hop wanaimba vitu vya msingi sana. Wasikilize Weusi, wasikilize Rostam, Fid Q, Nikki Mbishi, Mwana FA, Profesa J na wasanii wengine kisha wasikilize wale wa Bongofleva utauona tofauti zao.

Nilishasema sina lengo la kumshushia mtu heshima; ukweli mchungu ni lazima usemwe. Kwa nini kama hawa wasanii wa hip hop wanaonekana wana akili sana, lakini sokoni wanafeli? Kwanini wana uwezo mkubwa wa kulichambua soko la muziki la Bongo na dunia nzima, lakini ukirudi sokoni unakuta nafasi za juu zinashikiliwa na wale wale wa Bongofleva? 

Ukimsikiliza Wakazi akichambua kuhusu mikataba ya muziki unagundua anauelewa mkubwa, lakini ukirudi kumtafuta sokoni humkuti. Kwa nini?

Kwa nini licha ya kwamba wanaonekana wameelimika, lakini ndio wasanii wanaoongoza kwa kutokula matunda ya muziki wao.

Wasanii wa hip hop ndio wanaongoza kwa kulialia na kulalamika kwamba wanabaniwa. Ukiwakuta maskani wamejazana wanagongeana fegi na bapa la kinywaji utadhani sio wasanii ni wahuni fulani tu. Kwa nini iko hivyo? Au ndo mganga hajigangi? Kwamba wanajua kulichambua soko la muziki, lakini hawawezi kuchambua kwa nini wanafeli kupenya soko la muziki?

Au labda ndiyo kama ile midahalo ya shule unakuta kuna mada inasema “elimu ni bora kuliko pesa” ila upande wa utetezi wanakuja na pointi konki, lakini ni konki kwenye makaratasi kwenye uhasilia hazina maana hata kidogo?

Tatizo liko wapi? Wana hip hop wajitathimini muziki wao mzuri sana, waangalie wanapofeli.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags