Kelvin Kagambo
Ukitaja wasanii watano wakubwa wa kuimba Tanzania wanawake wapo. Ukitaja waigizaji wakubwa wa filamu Tanzania wanawake wapo.
Ukitaja madairekta wakubwa wa michezo ya kuigiza wanawake wapo. Ukitaja madansa wakubwa Tanzania wanawake wapo. Ukitaja maprodyuza wakubwa wa filamu Bongo wanawake wapo. Hii ni sawa na kusema wanawake wapo kila sehemu.
Hii ni tofauti sana na zamani. Zamani ilikuwa ukisikia mwanamke kwenye filamu jua ni muigizaji au mtu wa ‘make up’ ama anafanya mwendelezo (continuity).
Madairekta na maprodyuza walikuwa ni kina Steven Kanumba, Ray Kigosi, William Mtitu na wanaume wengine.
Na uzuri ni kwamba wanawake ambao wanakimbiza kwenye gemu zote mbili, muziki na filamu kwa sasa wako juu na wako juu sio kwa sababu ni wanawake, bali wapo juu kwa sababu wako vizuri kwenye wanachofanya.
Ukikutana na shabiki wa tamthilia anaizungumzia Jua Kali ya Leah Richard Mwendamseke ‘Lamata’ utaelewa ninachomaanisha. Au we’ mwenyewe si unaona magoma ya Zuchu na Nandy yanavyotikisa mtaani. Au video za kucheza za Angel Nyigu zinavyokimbiza.
Lakini wakati wanawake wanatusua kwenye maeneo mengine - kwenye maprodyuza wa muziki na madairekta wa video za muziki hali bado mbaya.
Huwezi kuamini mpaka leo muziki wa Bongo Fleva ukiwa na waimbaji wakubwa zaidi ya mia moja, lakini maprodyuza wakubwa wa muziki zaidi ya 20, madairekta wa video za muziki wakubwa takribani 20 na ukiingiza mabilioni ya pesa kwa wasanii na serikali lakini umekosa prodyuza hata mmoja wa kike na mwanamke hata mmoja anayefanya kazi kama mwongozaji wa video za muziki.
Hii inanifanya muda mwingine nitamani kama vipi Paula wa Kajala - mtoto wa P Funk akimaliza kulea mtoto wake na Marioo atulie akabidhiwe mikoba ya baba yake aokoe jahazi angalau tuwe na prodyuza wa kike kama ambavyo tunao madj kibao wa kike - kina Dj Sinyorita na Dj Mammy.
Madairekta kama kina Hanscana, Kenny na wenzao waangalie namna ya kuwavuta wanawake kwenye tasnia hiyo. Na maprdoyuza kama kina S2keezy na wenzao waangalie namna ya kuhakikisha mwaka hauishi bila Watanzania kusikia ngoma hata moja iliyotengenezwa na prodyuza wa kike.
Baadhi ya maprodyuza na madairekta wa video za muziki niliowahi kuongea nao wanasema wanawake wengi hawapendi kufanya kazi hizo mbili kwani walijaribu kuwafundisha wachache lakini wakaishia njiani. Binafsi sitaki kukubaliana nao.
Haiwezekani Tanzania ina wanawake zaidi ya milioni 30 akakosekana mmoja mwenye kiu kwelikweli ya kupenda kuwa prodyuza.
Huko mbele kuna kuna kinamama Sylvia Massy na wasichana wadogo kina WondaGurl wanafanya, kwanini Bongo isiwezekane? Tufanye kweli.

Leave a Reply