Master Jay afichua kinachowaponza wasanii wanaomiliki lebo
Mtayarishaji wa muziki nchini Joachim Marunda 'Master Jay' amesema rekodi lebo nyingi za wasanii Bongo zinashindwa kudumu na kufanya vizuri kutokana na mtaji mdogo.
"Msanii kama bado upo kwenye gemu alafu unafungua lebo lazima uwe na mtaji mkubwa wa kukuendesha wewe, lebo na wasanii wako. Isionekane hela nyingi zinaingia kwako alafu wasanii wanabaki nyuma. Unatakiwa uwekeze kote, siyo unawekeza kwako zikibaki ndiyo unaweka kwa wengine.
"Yaani mtaji unahitajika sana kwa soko la sasa ndiyo maana utaona lebo ambayo inafanya vizuri kila siku ni ya yule ambaye benki yupo vizuri. Huyo mtu sitaki kumtaja yaani ukimuangalia muda wote pesa ipo ana nguvu ya kuwekeza kwenye brand yake na wasanii wake,"amesema
Amesema hicho ni kitu ambacho wasanii wengi wanaomiliki rekodi lebo wanashindwa kukifanya.
"Ukiwa msanii ni mgogoro binafsi kuanzisha lebo, kwa sababu utaanza na wewe mwenyewe, lakini ukiwa vizuri inakuwa haina tatizo. Na hiyo ni changamoto ambayo unaona hawa wengine wanaipata hawawezi kushindana na hiyo lebo moja kwa sababu huyo yupo vizuri na ana njia zaidi ya moja ya kuingiza hela,"amemalizia Master Jay
Utakumbuka mwaka 2020 Shilole alitangaza kuanzisha lebo ya muziki inayoitwa Shishi Gang. Siku anatangaza lebo hiyo kwa mara ya kwanza ilikuwa pia ni siku ambayo alimtangaza ‘msanii wake’ anayeitwa Renzo.
Mpaka hivi sasa Renzo siyo msanii wa Shishi Gang tena, lakini Shishi Gang bado ipo na 2023 ilitambulisha msanii mpya anayeitwa Nice. Unawajua Renzo au Nice?
Mwaka 2016, Ommy Dimpoz alianzisha lebo yake ya muziki ya kuitwa PKP na alimtambulisha msanii anayeitwa Nedy Music. PKP hadi sasa watu wengi hawaifahamu.
Mwaka 2020 rapa Joh Makini alizindua lebo yake na kuipa jina la Makini Records. Wakati anazindua pia alimtambulisha ‘msanii wake’ anayeitwa Ottuc William, lakini kwa mujibu wa Instagram ya Ottuck haionyeshi kama bado ni msanii wa Joh Makini.
Alipotoka WCB, Harmonize alianzisha lebo yake ya Konde Gang, kisha akamsajili Ibraah na baadaye akaongeza wasanii wengine akiwemo Country Boy pamoja na kuwavuta wasanii waliokuwa wanafanya kazi Kings Record ya Alikiba, Cheedy na Killy.Mpaka dakika hii ni msanii mmoja tu aliyebaki Konde Gang kati ya wanne waliokuwapo.
Mwaka 2021 Rayvanny alizindua lebo yake inayoitwa Next Level Music na pia alimtambulisha MacVoice. Habari nzuri ni kwamba Macvoice bado yuko Next Level. Lakini kazi zake hazionekani mbali na hao wapo na wengine walioanzisha lebo lakini hadi sasa hatma zake hazifahamiki.

Leave a Reply