Tasnia ya sanaa nchini inatazamiwa kufanya mabadiliko baada ya kupitishwa kwa matumizi ya akili mnemba (Artificial Intelligence AI). Hatua ambayo inatarajiwa kuongeza ubunifu, thamani na kulinda kazi za kisanii.
Haya yanajiri baada ya Baraza la Sanaa la Taifa BASATA kufanya mkutano wa mashauriano na Taasisi ya Utafiti ya Kiafrika inayojihusisha na akili mnemba, African Research Institute for Artificial Intelligence (ARIFA) kuchunguza athari za AI katika sekta ya ubunifu.
Mkutano huo uliofanyika katika ofisi za BASATA, unaashiria mwanzo wa safari muhimu ya kuunganisha AI katika mandhari ya kisanii nchini.
Akizungumza na Mwananchi Machi 29, Katibu Mtendaji wa BASATA, Dk Kedmon Mapana, amewataka wasanii kukumbatia teknolojia ya AI zaidi kuliko kuiogopa.
"AI ipo na hatuwezi kuikwepa, ni suala la kwamba sasa sisi kama Baraza la Sanaa la taifa, tunalielewa kwa kina, linamanufaa gani, linahasara zipi, lakini pia wadau wetu ambao ndio wasanii, nao pia kuliewelewa hili jambo, kulikimbia sio solution.
“Wengine wanasema akili mnemba inakuja kuchukua kazi za watu, lakini pia sisi tunaweza kuliangalia kama ni fursa ya kurahisisha kazi"
Ameongezea kuwa itawasaidia wasanii kurahisha namna ya ufanyaji wa kazi hususani katika uandishi na utayarishaji wa nyimbo zao.
"Kama msanii alikuwa anatunga wimbo wake anachukua wiki moja namna gani anaweza kutumia akili mnembe kumsaidia. Unaweza ukamwambia alikuwa anaandika mashairi, kwa siku tatu au wiki nzima, lakini akili mnemba akisema anaomba mashairi nane basi inampa nane, akisema bwana punguza mengi matano, inampa matano, ukitaka matatu inakupa matatu.
"Lakini ikikwambia weka melodia hapo, inawezekana melodia ulikuwa huna, inakusaidia kuweka melodi, inakusaidia kukupa beat hapo, lakini ukisema kwamba mbona mimi sielewi hii vipi, hebu weka beat la mapigo sita kwa nane, au weka mapigo ya nne kwa nne, kwahiyo tusiikimbie"
Hata hivyo, Mapana amesema kuwa akili mnemba itawasaidia pia Basata katika kusimamia sekta ya sanaa kwa kutoa takwimu sahihi.
"Lakini akili mnembe inaweza kutusaidia sisi kama Basata tunasimamia hii sekta ya sanaa, lakini tunajuaje kama leo kuna matukio yanaendelea Mwanza ya sanaa, yanasaidia vipi, akili mnemba itusaidie kubainisha na kutafuta takwimu sahihi,”amesema
Naye msanii wa Bongo Fleva Mussa Mabumo, maarufu kama Bando Mc anaamini kuwa akili mnembe kama itatumika kwa usahihi itabadilisha namna ya utunzi wa muziki.
"Ikitekelezwa kwa usahihi, AI itasaidia katika kuunda nyimbo, kutoa mawazo mapya ya kisanii, na kuboresha ubora wa jumla wa kazi ya ubunifu," amesema Bando.
Bando Mc pia ameongezea kuwa AI inaweza kusaidia katika kuchanganua tabia ya mashabiki, kuwawezesha wasanii kuelewa watazamaji wao vyema.
Wakati huo huo, mkurugenzi mashuhuri wa video Derogations Abel alisisitiza kwamba AI inapaswa kutumika kama zana shirikishi badala ya kuchukua nafasi ya ubunifu wa mwanadamu.
"AI haiwezi kukufanyia kila kitu, lakini inaweza kufanya kazi yako iwe rahisi na ya haraka zaidi. Kwa mfano, kuandaa mwongozo huchukua muda, lakini zana zinazoendeshwa na AI zinaweza kusaidia kutengeneza mwongozo (script) katika muda mfupi zaidi," amesema.
Zana kadhaa za AI tayari zinatumiwa kurahisisha vipengele mbalimbali vya uzalishaji, na kufanya michakato ya ubunifu kuwa na ufanisi zaidi.

Leave a Reply