Kama humfahamu Hamisi Shabani a.k.a MacVoice naomba nikutambulishe; huyu ni msanii wa muziki wa Bongofleva kutoka Lebo ya Next Level Music ya Rayvanny.
Alitambulishwa 2021 baada ya Rayvanny kujitoa Wasafi na kuanzisha lebo yake hiyo.
Dogo anaimba vizuri. Ana ngoma kadhaa zilizobahatika kwenda mjini kama vile Nenda na Only You aliyoimba na Mbosso.
Kwa kifupi ana mashabiki wake, lakini vyote hivyo havijamzuia kuingia kwenye rekodi ya wasanii waliowahi kuchekwa kwa kufanya shoo za vichochoroni a.k.a shoo za chaka to chaka.
Iko hivi, juzi kulikuwa na video inazunguka mtandaoni ikimuonyesha Macvoice anaimba sehemu ambayo ni kama kwenye banda hivi.
Kwenye video hiyo watu walikuwa wakikomenti kwamba dogo alishafulia na sasa anafanya shoo za chaka to chaka, na wengine wakisema lebo yake ya Next Level imeshindwa kumsaidia mpaka anafikia kujidhalilisha kwa kwenye shoo za vichochoroni
namna hiyo.
Sitaki kuzungumzia tuhuma za lebo yake kushindwa kumuhudumia, lakini nakubaliana na waliokuwa wakikomenti. Ni kweli hali ya dogo kwenye gemu ni kama vile hahudumiwi vizuri. Hatoi ngoma, hasisiki, haeleweki
kama yupo au alishakata ringi. Yaani bado anajitafuta na kujipambania sana.
Kitu ambacho sikubaliani nacho ni mashabiki kumcheka kwamba anafanya shoo za vichochoroni kwani kusema ukweli kwa hali ya muziki wa Macvoice nadhani namba zinambeba kufanya shoo za vichochoroni. Twende kwenye namba.
Shoo za vichochoroni au chaka to chaka zimepata umaarufu mbaya siku hizi kwa sababu ya Instagram.
Unajua huko Instagram kila msanii anajifanya ni msanii mkubwa, msanii mwenye levo za juu na ni msanii wa kimataifa. Kwa hiyo mashabiki nao wanategemea kumuona kwenye shoo zilizokwenda shule, zinazoeleweka, za
kimataifa - yaani shoo zenye hadhi.
Lakini, ukweli ni kwamba sio wasanii wote wanabahatika kupata shoo za aina hiyo na hiyo inawafanya wakae muda mrefu bila kufanya shoo. Na shoo ni moja ya njia kuu ya msanii kujlingizia kipato. Kwa hiyo kama hafanyi shoo maana yake hapati pesa. Na hapo ndipo umuhimu wa shoo za chaka to chaka zinapoingia.

Leave a Reply