Ningekuwa S2Kizzy nisingefanya haya...

Ningekuwa S2Kizzy nisingefanya haya...

Ningekuwa S2Kizzy nisingebishana na mtu yeyote anayesema S2Kizzy sio prodyuza mkali. Nisingebishana na mtu yeyote anayekataa kukubali kwamba kati ya ‘hit song’ zote zilizotoka 2024 asilimia 80 zimetoka zimetengenezwa S2Kizzy.

Zaidi ningemkumbusha kwamba ngoma ya Dah pamoja na Dah Remix za Nandy zote zimetengenezwa na S2Kizzy, Mapoz ya Diamond, Nisiulizwe ya Jux, Number One ya Billnass na Mbosso, Romeo ya Darassa na Zuchu, Hakuna Matata ya Marioo, Nisiulizwe ya Jux na Komasava ya Diamond.

Ningekuwa S2Kizzy wala nisingebishana na wanaosema S2Kizzy anatengeneza hit song kwa sababu anafanya kazi na wasanii wakubwa. Zaidi ningewakumbusha kwamba, wasanii wakubwa, iwe Diamond, Alikiba, Nandy, Zuchu, Marioo, Harmonize na wengine huwa wanafanya kazi na prodyuza wengine wa muziki pia lakini mwisho wa siku hit song nyingi zinatoka mikononi mwa S2Kizzy.

Pia ningewakumbusha kwamba kitendo cha S2Kizzy kufanya kazi na maprodyuza wakubwa kinaonyesha wazi kwamba S2Kizzy ni prodyuza mkubwa. Hivyo ni haki ya S2Kizzy kujimwambifai.

Ningekuwa S2Kizzy nisingebishana na watu wanaoponda kipaji cha S2Kizzy kwa sababu najua Tanzania inaongozwa na kauli mbiu ya “hujafa hujasifiwa”. Ningekuwa S2Kizzy ningetambua kwamba Kibongobongo msanii unaonekana wa maana ukifariki dunia.

Nasema hivi kwa sababu nina uhakika, siku ambayo S2Kizzy atafariki, nyimbo zake zitapigwa siku nzima, masaa 24, bila mapumziko. Nina uhakika siku ambayo S2Kizzy atavuta pumzi yake ya mwisho kurasa za Instagram zitajaa picha zake na ‘kapsheni’ za kusadiki kwamba hatujawahi kuwa na prodyuza kijana aliyewahi kutoa hits nyingi kumzidi S2Kizzy.

Nina uhakika kwa sababu nimeyaona hayo yakitokea. Nimeshuhudia watu waliokuwa wakiponda Bongo movie ikiwemo filamu za Kanumba, jinsi walivyojazana kwenye msiba wake, jinsi walivyojiongelesha, na jinsi walivyozalisha msemo wa Kanumba amekufa na Bongo Movie, wakimaanisha Kanumba ndiye aliyekuwa anaibeba Bongo Movie. Lakini hawakusema hayo akiwa hai. Walimponda, walimpinga. Bongo husifiwi mpaka ufe.

Ningekuwa S2Kizzy nisingebishana na watu wanaosema S2Kizzy hana haki ya kujiita GOAT wa kizazi chake kwa sababu hajamtoa msanii mpya hata mmoja. Kwanini? Kwa sababu kumtoa msanii mpya inaweza kuwa moja ya kigezo cha kuwa prodyuza bora, lakini sio lazima kila prodyuza atoe msanii. Prodyuza kazi yake ni kutengeneza muziki. Kutoa msanii ni nyongeza tu.

Ningekuwa S2Kizzy nisingebishana na watu wanaosema S2Kizzy hana sababu ya kujiita GOAT kwani anatengeneza Amapiano tu. Sasa kama wateja wake, wasanii wanataka biti za Amapiano yeye afanyaje? Awape taarab. Pia sio kauli ya ukweli ukizingatia ngoma tulizozitaja pale juu, Amapiano ni moja tu.

Kwa kifupi ni kwamba, S2Kizzy ni mmoja wa maprodyuza wakubwa sana na ninadhani ana haki kujiita vyovyote anavyotaka. Jamaa ametengeneza hits na wasanii wengi zaidi ya prodyuza yeyote wa kizazi chake Bongo na kama hiyo haitoshi kumfanya mtu ajiite GOAT, niambie nini kinatosha?






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Christina Lucas


Latest Post

Latest Tags