Jina Nay wa Mitego lilianza hivi

Jina Nay wa Mitego lilianza hivi

Msanii wa Hip Hop Bongo, Nay wa Mitego alikuja na mtindo wa aina yake kwenye muziki kwa kukosoa wasanii wengine na baadhi ya mambo kwenye tasnia jambo lililompatia umaarufu kutokana na kuonekana kama jeuri.

Tayari ameanzisha lebo yake, Free Nation, akishinda Tuzo za Muziki Tanzania (TMA), ametoa albamu moja Rais wa Kitaa (2022), huku tungo na misimamo yake katika baadhi ya mambo vikiiba chapa yake kwa miaka yote. Fahamu zaidi.

Mara ya kwanza Nay wa Mitego kuingia studio ilikuwa 1998 katika studio inaitwa Marimba na alilipa Sh7,000 kwa ajili ya kurekodi, lakini hakufanikiwa kutoka kimuziki wakati huo.

Hata hivyo, hakukata tamaa kwani baadaye alirekodi Bongo Records kwa P-Funk Majani na Mawingu Studio kwa DJ Boni Luv ambapo wasanii kama Mwana FA na Gangwe Mobb wametokea.

Kabla ya 2005, Nay wa Mitego alikuwa hatumii jina hilo, bali alikuwa anaitwa ‘Nay’ jina alilopewa na mpenzi wake, ila alipotoa wimbo uitwao Wamitego na kufanya vizuri ndipo mashabiki wengi wakampa jina la Nay wa Mitego.

Msanii wa kwanza maarufu Bongo kwa Nay wa Mitego kukutana naye alikuwa ni hayati John Mjema maarufu kama Bomba la Mvua aliyefariki Februari 2008 baada ya kutamba sana kupitia wimbo wake, Wachumba 30.

Akiwa kidato cha kwanza ndipo Nay wa Mitego alirekodi wimbo na kuutoa rasmi uitwao Kama Unanipenda (2001) ambao ulitayarishwa na P-Funk Majani huku gharama za studio akilipiwa na mpenzi wake kipindi hicho.

Katika historia ya msanii huyu ni ngumu kuuacha ugomvi wa Nay wa Mitego na Madee uliosababisha kuanza kuchapana katika nyimbo, ugomvi ambao haukuanza kipindi Nay ametoka kimuziki, bali mtaani kwao, Manzese ambapo wote wawili walikuwa na kambi zao.

Kambi ya Nay wa Mitego ilikuwa inaitwa Small Tiger, huku Madee akiongoza kikosi chake, World Camp Nakoz Camp. Huko ndipo upinzani wao ulianza kisha kuja kuhamia kwenye muziki wa Bongofleva.

Hata hivyo fahamu kuwa tangu Nay wa Mitego aanze muziki hajawahi kuchagua mrembo (video vixen) ili atokee kwenye video ya wimbo wake, bali kazi hiyo mara zote humwachia mwongozaji wa video husika ambaye anatayarisha kazi husika.

Ikumbukwe chanzo cha bifu la Gigy Money na Nay wa Mitego lilianza baada ya Gigy kulipwa Sh20,000 kutokea kwenye video ya wimbo wa Nay ‘Shika AdabuYako’ kama video vixen, malipo ambayo yalikuwa tofauti na makubaliano yao.

Utakumbuka Nay alimshirikisha Diamond kwenye wimbo wake, Muziki Gani (2013) ambao ulifanya vizuri na kumuongezea mashabiki wengi hasa wa kike na kumpatia dili kutoka moja ya kampuni za simu za mkononi.

Baadaye Nay akaona kufanya kolabo na Diamond ni bidhaa inayouzika kwa urahisi ndipo wakaachia wimbo mwingine, Mapenzi au Pesa (2016) ingawa haukuweza kufanya vizuri kama ule wa mwanzo na hata video yake hawakuitoa.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Christina Lucas


Latest Post

Latest Tags