Marcus Abba anashtumiwa na baba yake mkubwa, Douglas Mayanja 'Weasel' ambaye pia ni mwanamuziki kwa kumkosoa baba yake mzazi, Jose Chameleone kutokana na mtindo wake wa maisha.
Weasel alionekana kutopendezwa na kitendo cha Marcus kuzungumza hadharani kuwa baba yake ni mlevi wa pombe lakini pia akahoji ni vipi mlevi akumbuke kulipa ada ya shule ya Abba Marcus yenye thamani ya dola 20,000 sawa na Sh73 milioni.
"Huyo mtu unayemwita mlevi amefadhili elimu yako kwa miaka mingi akakupeleka Marekani akakununulia nyumba huko huku akiendelea kukulipia bili zote inauma kwa sababu ni baba yako. Nakupenda Abba lakini tafadhali acha,” alisema Weasel.
Hata hivyo Marcus hakutaka shutma hizo zipite badala yake alijibu kuwa huo ni wajibu wa mzazi kusomesha mtoto.
"Chameleone hapaswi kupongezwa kwa kutulipia ada ya shule. Niwajibu wake na hatujawahi kumuomba atulete duniani," amesema Marcus.
Kwa sasa Chameleone yupo nchini Marekani ambapo alisafirishwa na Rais wa Uganda, Yowery Museveni siku ya Jumatatu Desemba 23, 2024 na inaelezwa kuwa msanii huyo ameamua kuwa mbali na hajibu ujumbe anaotumiwa na mwanaye tangu alipotoa taarifa hadharani kuhusu maradhi ya Kongosho yanayomsumbua kwa kipindi kirefu ambayo yamesababishwa na uraibu wa pombe kali.
Utakumbuka kuwa taarifa za kuumwa kwa Chameleone zilianza kusambaa kwenye mitandao ya kijamii wiki iliyopita baada ya mtoto huyo kuweka wazi kuwa baba yake anasumbuliwa na maradhi ya kongosho (Acute Pancreatitis) yaliyosababishwa na uraibu wa pombe.
Leave a Reply