Vituko vya Bongo Movie enzi hizo

Vituko vya Bongo Movie enzi hizo

Wakati wanaanza Bongo Movie enzi hizo ilikuwa vituko tu. Mtu anaigiza kama malaika, halafu anamwambia mwenye shida kuwa: "Usijali, Mungu wa mbinguni atakusaidia." Malaika gani wa hivi?

 Risasi inachukua nusu saa kumfukia adui. Mlio wake ama njiti ya kiberiti. Ikimpata kifuani damu inatoka kama ile ya kipimo cha malaria. Anaangalia sehemu ya kuangukia ili asiumie.

 Kahaba ilikuwa lazima avute sigara, jambazi lazima avae koti refu jeusi na miwani ya giza. Mganga lazima awe porini, mchafu na anaongea kwa ukali ukali. Jini likivuka barabara linaogopa bodaboda. 

 Komediani yeyote lazima awe mlinzi. Tena awe fyatu fyatu asiyejielewa. Hii ni kwa kila filamu. Ilikuwa kawaida msanii kuvaa shati moja filamu tatu au nne tofauti. 

 Filamu inaongelea mwaka 1977, ofisini picha ya Rais Kikwete. Na wimbo unaosikika ni Starehe wa Ferous. Na kila anayechomwa kisu lazima iwe tumboni tu. 

 Unakaa na 'rimoti', 'sini' ya kugombana sauti inapaa. Ugomvi ukiisha sauti inashuka inabidi uongeze tena. Wakiigizia juani kivuli cha 'maiki' au maiki yenyewe inatokea. 

 Mwanasheria wa kike mahakamani ana nguo za kutokea usiku. Kituo cha polisi ni kimoja tu kwenye muvi zote. Polisi wakijitambulisha utasikia: "Sisi ni askari polisi kutoka kituo cha kati". 

 Anayeigiza kuelezea habari zake za maisha yake ya nyuma. Atanyanyua uso juu, kamera itaonesha macho yake. Atasogea dirishani huku kakunja mikono kifuani. Hii ni kwa filamu zotee.

 Mume na mke wapo ndani, ukutani kuna picha ya mume na mke ambao hawapo kwenye filamu. Na mapenzi ni lazima masikini apendwe na tajiri. Kazi za filamu sasa zipo mbali sana. Kila kitu kipo super.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Christina Lucas


Latest Post

Latest Tags