Mahakama ya Coroner ya Ikorodu, Lagos, Nigeria, imetoa ripoti rasmi kuhusu chanzo cha kifo cha mwanamuziki Ilerioluwa Aloba, maarufu kama Mohbad aliyefariki dunia Septemba 12, 2023.
Mahakama hiyo jana Ijumaa, Julai 11, 2025, imesema kuwa kifo cha Mohbad kilitokana na athari kali ya mzio (allergic reaction) baada ya kupewa dawa kupitia sindano na daktari ambaye hana leseni.
Kwa mujibu wa ripoti ya daktari mtaalamu wa uchunguzi wa miili, Dr. Eze Uwom Okereke, ambaye aliwasilisha ushahidi mahakamani, vipimo vilionesha kuwa hakukuwa na dalili za matumizi ya dawa za kulevya au sumu mwilini mwa marehemu.
Mahakama ilieleza kuwa siku ya tukio, Mohbad alilalamika kuwa anahisi maumivu na aliitwa nesi aitwaye Feyisayo Ogedengbe, ambaye hakuwa na leseni halali ya kutibu. Inadaiwa nesi huyo alimchoma sindano aina ya Tetanus Toxoid na Ceftriaxone, bila uangalizi wa daktari, baada ya muda mfupi, Mohbad alianza kupata mshituko na kupoteza fahamu.
Uchunguzi wa kitabibu ulieleza kuwa jeraha dogo alilokuwa nalo kwenye mkono halikuwa na mchango wowote katika kifo chake. Badala yake, kifo chake kilielezwa kuwa kilisababishwa na “medical misadventure,” yaani hali ya kupoteza maisha kutokana na tiba isiyo sahihi.]
Kutokana na ushahidi huo, Mahakama ilipendekeza hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya nesi huyo kwa kutoa huduma za afya bila kibali halali, jambo linalochukuliwa kama kosa la jinai nchini Nigeria.
“Kwa mujibu wa kifungu cha 29 cha sheria ya Coroner ya Jimbo la Lagos, mahakama hii inapendekeza kuwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) ianze mara moja mchakato wa kumshtaki Felicia Ogedengbe kwa kutoa huduma za matibabu kinyume cha sheria na kwa uzembe mkubwa,”imeeleza mahakama hiyo
Kwa sasa, familia ya Mohbad na mashabiki wanasubiri hatua zaidi kutoka kwa Ofisi ya Mashtaka ya Umma (DPP) kuhusu hatima ya kesi hiyo na iwapo watamfungulia rasmi mashtaka ya jinai nesi huyo.
Leave a Reply