Hatimaye filamu maarufu ya Korea Kusini iitwayo Squid Game msimu wa pili inaachiwa rasmi leo Desemba 26, 2024.
Msimu huu mpya wa Squid Game unatarajiwa kumuonesha mshindi wa awali, Seong Gi-hun (Lee Jung-jae), akirudi kwenye uwanja wa mashindano ikiwa ni miaka mitatu baada ya kushinda kwake zawadi ya Sh45.6 bilioni.
Lakini katika msimu huu, itaonesha mwigizaji huyo akiwa na lengo lingine tofauti na fedha kama ilivyokuwa awali.
"Miaka mitatu baada ya kushinda Squid Game, Mchezaji namba 456 alikataa kwenda Marekani na anarudi na azimio jipya akilini mwake," umeeleza muhtasari wa msimu wa pili.
Msimu mpya wa Squid Game utakuwa na mastaa kama Lee Jung-jae, Lee Byung-hun, Wi Ha-jun, na Gong Yoo. Huku kukiwa na washiriki wapya kama Yim Si-wan, Kang Ha-neul, Park Gyu-young, Lee Jin-uk, Park Sung-hoon, Yang Dong-geun, Kang Ae-sim, Lee David, Choi Seung-hyun, Roh Jae-won, Jo Yu-ri, na Won Ji-an.
Utakumbuka msimu wa kwanza wa Squid Game ulishinda tuzo sita za Primetime Emmy, ikiwemo tuzo ya kihistoria kwa mkurugenzi Hwang Dong-hyuk, ambaye alishinda tuzo ya Outstanding Directing kwa Drama Series. Waigizaji Lee Jung-jae na Lee You-mi pia walishinda tuzo kwa ufanisi wao.
Pia filamu hiyo imetazamwa zaidi duniani kupitia Netflix, huku ikiwa imetazamwa zaidi ya mara bilioni 1.6. Leo Squid Game inaachiwa ikiwa ni takribani miaka mitatu tangu kuachiwa kwa mara ya kwanza.
Leave a Reply