Moja ya filamu ambayo katika msimu wa sikukuu za mwisho wa mwaka huchuka nafasi kubwa katika maisha ya watu ni ‘Home Alone’.
Ufuatiliwaji wa filamu hiyo kila mwaka umekuwa ukipelekea kuvuna mamilioni ya fedha, kutokana na maudhui yake kuendana na msimu huu.
Home Alone ni filamu iliyotoka Novemba 16, 1990 huku lengo la kutengenezwa kwake likiwa ni kuhamasisha watu kuondokana na msongo wa mawazo katika kipindi cha likizo na sikukuu za mwisho wa mwaka.
Kulingana na James, mtoto wa mwandishi wa filamu hiyo na mtayarishaji wa Home Alone, John Hughes, alifunguka kuwa wazo la kutengeneza filamu hiyo kwa baba yake lilikuja baada ya familia yao kuwa na likizo mbaya mwaka 1989.
Filamu ya kwanza katika mfululizo wa Home Alone iliyoongozwa na Chris Columbus ilichezwa na mwigizaji nguli kutoka Marekani, Macaulay Culkin ambaye aliingiza kama Kevin McCallister, mvulana mdogo anayelinda nyumba yao iliyopo mitaa ya Chicago, dhidi ya uvamizi wa majambazi wawili baada ya familia yake kumsahau wakati wa likizo yao ya Krismasi ya kwenda Paris.
Mauzo ya Home Alone
Toleo la kwanza la filamu hiyo lililotoka mwaka 1990 lilikuwa na bajeti ya dola 18,000,000 na ilifanikiwa kupata mapato ya ndani dola 285,761,243 huku mapato ya Kimataifa yakiwa ni dola 3,164,185. Hata hivyo filamu hiyo ilipata mapato ya dola 285.7 milioni Amerika Kaskazini yakiwa ni mapato ya juu zaidi katika filamu hiyo.
Aidha Home Alone: Lost in New York 2 & 3 ilifanikiwa kupata ya dola 173,585,516 na dola 30,882,515, mbali na kupata maokoto katika mauzo ya filamu hizo, pia ziliwabadilishia maisha baadhi ya mastaa akiwemo Macaulay Culkin aliyeigiza kama muhusika mkuu ambaye alilipwa dola 100,000 na dola 4.5 milioni (Home Alone 2) katika jukumu lake hilo.
Nyumba iliyoigiziwa Home Alone yauzwa
Mbali ya kuwa na kumbukumbu nzuri, nyumba ambayo ilitumika kuigizia filamu ya Home Alone yenye vyumba vitano vya kulala, bafu sita, na uwanja wa michezo na sehemu ya kutazama sinema iliyopo katika kitongoji cha Winnetka, Illinois Chicago imeuzwa Mei 2024.
Nyumba hiyo ambayo iliwekwa katika tovuti za uuzaji wa bidhaa mbalimbali zisizo hamishika ya ‘Coldwell Banker Realty's Dawn McKenna Group’ iliripotiwa na tovuti ya ABC7 kuuzwa kwa dola 5.25 milioni ikiwa ni zaidi ya Sh 13.6 bilioni.
Awali nyumba hiyo ilikuwa ikimilikiwa na John na Cynthia Abendshien ambao waliiuza kwa mara ya kwanza mwaka 2012 kwa Tim na Trisha Johnson ambapo wawili hao pia waliiamua kuiuza mapema mwaka huu, huku mnunuaji wa awamu ya mwisho akiwa hajatambulika jina lake mpaka sasa. Aidha kwa mujibu wa tovuti mbalimbali nyumba hiyo imebadilishwa muonekano na kufanywa mpya.
Macaulay Culkin ‘Kelvin’ (Muhusika mkuu Home Alone)
Akiwa na umri wa miaka 10 alikabidhiwa jukumu hilo la uhusika mkuu katika filamu hiyo iliyoiteka dunia kwa karne kadhaa. Mpaka kufikia sasa mwigizaji huyo amekuwa akifanya vizuri kupitia filamu mbalimbali zikiwemo Changeland, Party Monster na nyinginezo.
Kutokana na kuitendea haki tasnia ya filamu, Desemba 2023 mwigizaji huyo alitunukiwa tuzo ya heshima ya Hollywood Walk of Fame kufuatia na makubwa aliyoyafanya katika tasnia ya filamu nchini humo.
Aidha kufuatia minong’ono katika mitandao ya kijamii kuhusiana na kushindikana kutolewa muendelezo wa Home Alone hatimaye mwigizaji huyo ambaye kwa sasa ana miaka 44 ametangaza kuja kivingine msimu huu wa sikukuu za mwisho wa mwaka 2024 ambapo kupitia ukurasa wake wa Instagram amechapisha tangazo kuwa mwishoni mwa mwaka huu hatowaacha tena mashabiki zake kinyonge.
Leave a Reply