Katika pitapita zangu kwenye mitandao ya kijamii mapema leo Februari 26, 2025 nikakutana na video inayomuonesha mwanamuziki Alikiba akisalimiana na Harmonize kwa kukumbatiana wakiwa kisiwani Unguja ambapo tuzo za Trace zinagawiwa leo.
Lakini katika salamu zile Harmonize alijaribu kuvua mkufu wake wa shingoni na kutaka kumvalisha Alikiba lakini hakufanikiwa.
Video hiyo inaendelea kwa kumuonesha Alikiba akikataa mkufu ule huku akikimbia lakini upande wa pili anasikika msanii wa Kenya Bien akishangaa ukubwa wa mkufu ule. Kisha Harmonize ikabidi abadili mawazo na kumvalisha Bien.
Tukio hili linanikumbusha matukio kadhaa yaliyowahi kutokea kwenye kiwanda cha burudani duniani kutoka kwa mastaa mbalimbali.
Tukio kama hilo linataka kufanana na lile la Jay-Z na Nas, katika vita yao iliyoanza kwa Jay-Z kutunga wimbo maalumu wa kumshambulia Nas ulioitwa 'Takeover'. Kisha Nas alijibu kwa kutunga wimbo uitwao 'Ether'. Kutokana na mvutano huo Nas aliweka wazi kuwa hatotumia bidhaa yoyote ambayo itahusiana na Jay-Z wala kushirikiana na wasanii wa upande wake.
Aidha kwa 50 Cent na Ja Rule, mahasimu hawa ambao ugomvi wao ni wa miaka na miaka ulisababisha 50 Cent na wafuasi wake kutokubali kuvaa au kutumia bidhaa zinazohusiana na Ja Rule.
Cardi B na Nicki Minaj nao wamewahi kuwa kwenye mvutano uliopelekea, Cardi B kujitenga na Nicki Minaj na kuonyesha wazi kuwa hataki kuhusiana na bidhaa au mtindo wowote unaomuhusu Nicki.
Hao ni baadhi ya wasanii niliowakumbuka baada ya kuona video ya Konde Boy na Mfalme. Lakini kikubwa ni video hiyo inaonesha namna ambavyo msanii anatakiwa kulinda chapa (Brand) yake binafsi hasa katika biashara ya muziki.
Utakumbuka Harmonize amewahi kuwa msanii katika lebo ya WCB inayomilikiwa na Diamond ambaye anatazamwa kama mpinzani mkubwa wa Alikiba. Lakini Harmonize alijitoa kwenye lebo hiyo mwaka 2019 na kuamua kuanzisha lebo yake ya muziki Konde Music Worldwide iliyokuwa na wasanii Ibraah, Country Boy, Anjella,Cheed na Killy ambapo kwa sasa amebaki Ibraah pekee
Hata hivyo katika wasanii wawili Cheed na Killy waliokuwa Konde Gang, walitoka kwenye lebo ya Alikiba, Kings Music. Lakini wawili hao hata baada ya kwenda Konde Gang nako waliondoka pia. Hivyo ni ngumu kujiaminisha kuwa kuna urafiki mkubwa kati ya Harmonize na Alikiba hadi kufikia hatua ya kuvalishana mkufu.
Mbali na hayo hivi ni vitu vingine vinavyoweza kuwa sababu ya Alikiba kukataa cheni ya Harmonize
Kulinda chapa yake, msanii yeyote yule aliyepo kwenye mikono au anasimamia lebo fulani ni muhimu kulinda lebo yake. Alikiba kuvaa cheni ya Konde ni kuonesha udhaifu hasa katika lebo yake ya Kings Music. Hasa ukizingatia cheni hiyo ina utambulisho wa Konde Music Worldwide (KMW)
Kiba kuvaa cheni Konde wakati mwingine kunaweza kuleta utata kuhusu msanii mwenyewe hasa kutoka kwa mashabiki wanaweza kuona kama ni kitendo cha kujidhoofisha.
Utakumbuka mwaka 2021 wakati Alikiba akifanya mahojiano na waandishi wa habari alimkataa Harmonize na kudai hana urafiki nae.
"Harmonize sio rafiki yangu wa karibu na wala sio rafiki yangu. Mimi nimekutana naye mara moja tu. Lakini vilevile nisingependa kumzungumzia kwa sababu hatuna mazoea ila ni msanii mwenzangu mtanzania ambaye anawakilisha vizuri Bongo Fleva,"alisema Alikiba

Leave a Reply