Mapya Yaibuka Kesi Ya Tupac, Snoop Dogg Atajwa

Mapya Yaibuka Kesi Ya Tupac, Snoop Dogg Atajwa

Aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Death Row Records, Suge Knight, amemshtumu Snoop Dogg kwa kujaribu kumdhamini Duane “Keefe D” Davis ambaye ni mtuhumiwa mkuu katika mauaji ya rapa Tupac Shakur.

Wakati alipokuwa kwenye mahojiano na ‘The Art of Dialogue’, Knight ameweka wazi kuwa huwenda Snoop ameamua kumdhamini Keefe D kutokana na wasiwasi alionao kuhusu mtuhumiwa huyo kufichua kuwa naye anahusika katika kifo cha Pac.

“Tangu nimekuwa hapa, Snoop na watu wengine wamekuwa wakijaribu kumdhamini huyo jamaa, Keefe D, kwa sababu anazungumza sana. Hata walimtuma mtu aje kuzungumza na mimi na kuniambia, "Hey! unaweza kumsaidia atoke huru". Nikasema sina uhusiano wowote na hilo na siondoki gerezani ili kwenda kwenye jela ya kaunti ya mtu yeyote,” amesema Knight

Knight, ambaye ametumikia muda mrefu gerezani kwa kosa la kuua bila kukusudia anaeleza kwamba kadri Keefe D anavyozidi kuzungumza, ndivyo watu wengi zaidi wanaweza kuhusishwa kama waliompinga Pac au walioshiriki katika kifo chake.

“Kwa jinsi inavyoonekana, Keefe D anasema kila kitu, unajua ninamaanisha nini?. Na kadri anavyozidi kuzungumza, ndivyo watakavyozidi kuathirika na hali hii,” amesema Knight

Aidha Knight alimshutumu moja kwa moja Snoop Dogg, akidai kwamba Ray J aliwahi kumwambia kuwa Snoop alijigamba kwake kuhusu madai ya kuhusika kwake katika kifo cha Shakur.

Inaelezwa kuwa Knight kwa muda mrefu amekuwa na uhusiano mbaya na wana hip-hop na mara nyingi ameonyesha kutoamini wale waliokuwa na uhusiano wa kibiashara na Tupac alipokuwa Death Row Records.

Utakumbuka Tupac Shakur alizaliwa 16 Juni 1971 na alifariki dunia 13 Septemba 1996 kutokana na majereha ya risasi baada ya kushambuliwa 7 Septemba 1996 huko Las Vegas, Nevada. Huku mastaa kadhaa wakuhusishwa katika mauaji hayo akiwemo Diddy, Snoop na wengineo.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags