Unaweza kusema ni bahati ya kipekee iliyoishukia Tanzania kwa mara nyingine tena. Achana na mashindano ya AFCON 2027 ambayo pia yatafanyika Tanzania. Kwa sasa ni tukio la burudani la Tuzo za Muziki Trace ambazo kwa mara ya zinafanyikia Zanzibar.
Tuzo hizo ambazo zinafanyika kwa mara ya pili tangu kuanzishwa kwake. Zilipoanzishwa zilifanyika Kigali nchini Rwanda na kwa sasa zinafanyika Zanzibar kisiwani Unguja ambapo leo hii wasanii mbalimbali wataondoka na tuzo zao.
Akitoa sababu za tuzo hiyo kufanyika kisiwani Unguja Seven Mosha ambaye ni mmoja wa waandaji wa tukio hilo amesema lengo la Trace ni kuonesha tamaduni na uhasilia ndiyo maana Zanzibar imefaa zaidi.
"Trace inasimamia muziki na utamaduni. Rwanda ilifanyika kwenye ukumbi wa ndani lakini 'vision' ya Trace yenyewe kama inaenda kila nchi ya Afrika ni kuangalia asilia na kufanyika nje. Sehemu ambayo inaonesha mandhari ya kila sehemu.
"Kwa hiyo tulivyokuwa tunafikiria ilikuwa ifanyike Serengeti lakini sasa kwenda huko ni ndege ndogondogo. Location yenyewe wasanii au ma-CEO wasingeweza kupanda ndege ndogo. Lakini jingine ilikuwa ni ndege ngapi ambazo zinatoka kimataifa zinatua pale. Hivyo ni vitu vilivyofanya Zanzibar ionekane bora zaidi,"amesema Seven
Hata hivyo Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar Mudrick Soraga amesema sababu nyingine zilizofanya tuzo hizo kufanyika Zanzibar ni upekee wa kisiwa hicho.
"Zanzibar kwa sasa iko juu kwa upande wa utalii na matukio makubwa. Kila taasisi, kila mtu anatamani kuwa kwenye kisiwa hiki. Upekee wa kisiwa hiki ndio umeweza kutoa msukumo kwa tukio kama Trace Music Awards kufanyika hapa. Na kwa habari tu, Zanzibar hivi karibuni ilitambuliwa kama moja ya maeneo bora kwa ajili matamasha,"amesema.
Ikumbukwe leo Februari 26,2025 jukwaa litatawaliwa na wasanii wazawa akiwemo Diamond Platnumz, Jux, Zuchu, Harmonize, Alikiba, Marioo, Abigail Chams, Mbosso, Lunya, Bella Kombo na Nandy. Mbali na hao wapo wasanii kutoka nje ya Tanzania kama Rema, TitoM & Yuppe, Joé Dwèt Filé, Fally Ipupa, Didi B, Tyler ICU, Qing Madi, Bien, Innoss’B, Yemi Alade, Black Sherif na wengineo.
Aidha tuzo hizo zitawakutanisha wasanii zaidi ya 300 wa kimataifa huku wakitoana jasho katika vipengele mbalimbali. Diamond anakuwa msanii pekee kutoka Bongo anayewania tuzo hizo katika kipengele cha 'Song Of The Year' kupitia ngoma ya 'Komasava'.
Diamond atachuana na Tyler ICU & Tumeloza ft. DJ Maphorisa, Nandipha808, Ceeka RSA, Tyron Dee – Mnike, Asake & Travis Scott – Active, Tam Sir ft. Team Paiya, Ste Milano, Renard Barakissa, Tazeboy, PSK - Coup Du Du Marteau, TiTom & Yuppe - Tshwala Bam, Tems - Love Me Jeje, Burna Boy – Higher, Rema & Shallipopi - Benin Boys na Tyla – Jump.

Leave a Reply