Mpenzi wa Ney alivyomlipia kurekodi wimbo wa kwanza

Mpenzi wa Ney alivyomlipia kurekodi wimbo wa kwanza

Msanii wa Hip Hop Bongo, Nay wa Mitego alikuja na mtindo wa aina yake kwenye muziki kwa kukosoa wasanii wengine na baadhi ya mambo kwenye tasnia jambo lililompatia umaarufu kutokana na kuonekana kama jeuri.

Tayari ameanzisha lebo yake, Free Nation, akishinda Tuzo za Muziki Tanzania (TMA), ametoa albamu moja Rais wa Kitaa (2022), huku tungo na misimamo yake katika baadhi ya mambo vikiibeba chapa yake kwa miaka yote. Fahamu zaidi.

Mara ya kwanza Nay wa Mitego kuingia studio ilikuwa 1998 katika studio inaitwa Marimba na alilipa Sh7,000 kwa ajili ya kurekodi, lakini hakufanikiwa kutoka kimuziki wakati huo.

Hata hivyo, hakukata tamaa kwani baadaye alirekodi Bongo Records kwa P-Funk Majani na Mawingu Studio kwa DJ Boni Luv ambapo wasanii kama Mwana FA na Gangwe Mobb wametokea.

Msanii wa kwanza maarufu Bongo kwa Nay wa Mitego kukutana naye alikuwa ni hayati John Mjema maarufu kama Bomba la Mvua aliyefariki Februari 2008 baada ya kutamba sana kupitia wimbo wake, Wachumba 30.

Akiwa kidato cha kwanza ndipo Nay wa Mitego alirekodi wimbo na kuutoa rasmi uitwao Kama Unanipenda (2001) ambao ulitayarishwa na P-Funk Majani huku gharama za studio akilipiwa na mpenzi wake kipindi hicho.

Kabla ya 2005, Nay wa Mitego alikuwa hatumii jina hilo, bali alikuwa anaitwa ‘Nay’ jina alilopewa na mpenzi wake, ila alipotoa wimbo uitwao Wamitego na kufanya vizuri ndipo mashabiki wengi wakampa jina la Nay wa Mitego.

Ugomvi wa Nay wa Mitego na Madee uliosababisha kuanza kuchapana katika nyimbo haukuanza kipindi Nay ametoka kimuziki, bali mtaani kwao, Manzese ambapo wote wawili walikuwa na kambi zao.

Kambi ya Nay wa Mitego ilikuwa inaitwa Small Tiger, huku Madee akiongoza kikosi chake, World Camp Nakoz Camp. Huko ndipo upinzani wao ulianza kisha kuja kuhamia kwenye muziki wa Bongofleva.

Nay wa Mitego aliamua kutoa wimbo wake ‘Mwanamke Hapigwi’ kwa ajili ya mama yake mzazi ambaye alikuwa anapigwa na baba yake hadi kushindwa kwenda kazini jambo lililokuwa linamkera rapa huyo.

Tangu Nay wa Mitego aanze muziki hajawahi kuchagua mrembo (video vixen) ili atokee kwenye video ya wimbo wake, bali kazi hiyo mara zote humwachia mwongozaji wa video husika ambaye anatayarisha kazi husika.

Ikumbukwe chanzo cha bifu la Gigy Money na Nay wa Mitego lilianza baada ya Gigy kulipwa Sh20,000 kutokea kwenye video ya wimbo wa Nay ‘Shika AdabuYako’ kama video vixen, malipo ambayo yalikuwa tofauti na makubaliano yao.

Wimbo wa Diamond Platnumz, Waka (2017) ambao amemshirikisha Rick Ross kutoka Marekani umechukua baadhi ya vionjo kutoka kwenye wimbo wa Nay wa Mitego, Makuzi (2017).

Cha kushangaza nyimbo zote mbili zilikuja kufungiwa na Baraza la Sanaa Taifa (Basata) na kutotakiwa kuchezwa kwenye vyombo vya habari kutokana na kukiuka maadili.

Utakumbuka Nay alimshirikisha Diamond kwenye wimbo wake, Muziki Gani (2013) ambao ulifanya vizuri na kumuongezea mashabiki wengi hasa wa kike na kumpatia dili kutoka moja ya kampuni za simu za mkononi.

Baadaye Nay akaona kufanya kolabo na Diamond ni bidhaa inayouzika kwa urahisi ndipo wakaachia wimbo mwingine, Mapenzi au Pesa (2016) ingawa haukuweza kufanya vizuri kama ule wa mwanzo na hata video yake hawakuitoa.

Namba 966 ambayo Nay wa Mitego amekuwa akiitaja sana kwenye nyimbo zake haina maana yoyote ingawa baadhi ya watu wamekuwa wakiihusisha na aina fulani ya imani, pia katika namba hizo, namba 6 ndio yenye umuhimu zaidi kwake.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Christina Lucas


Latest Post

Latest Tags