Hatimaye Liam Neeson Kapenda Tena

Hatimaye Liam Neeson Kapenda Tena

Mwigizaji mkongwe wa Marekani, Liam Neeson (73) anaripotiwa kuzama katika uhusiano mpya na mwanamitindo, Pamela Anderson (58) licha ya hapo awali kudai amefunga ukurasa huo kufuatia kifo cha mkewe, Natasha Richardson.

Liam ambaye amefanya vizuri katika filamu nyingi ikiwemo Made in Italy (2020), mwaka uliopita katika mahojiano na Jarida la People alisema amekata tamaa na mapenzi kutokana na kile alichotaja kama kumalizana na mambo hayo!.

Staa huyu alikuwa amemuoa mwigizaji wa The Parent Trap, Natasha Richardson kuanzia mwaka 1994 hadi 2009 alipofariki akiwa na umri wa miaka 45. Mwaka mmoja baada ya kifo cha Richardson, Liam alianzisha uhusiano na Freya St. Johnston wa Uingereza ila miaka miwili baadaye waliachana.

Baada ya miaka kadhaa ya upweke, Liam anatajwa kupenda tena na awamu hii yupo na Pamela Anderson ambaye wamecheza pamoja filamu mpya, The Naked Gun (2025).

Kwa mujibu wa chanzo kilichofanya kazi nao kwenye filamu hiyo, kimeueleza mtandao wa People kuwa ni uhusiano ya kweli, na inaonekana wazi kuwa wamevutiwa sana wao kwa wao.

Hilo lilidhihirika kwenye ziara yao ya kimataifa ya kuitangaza filamu hiyo. Walipokuwa kwenye kipindi cha Today siku ya Jumanne, Julai 29, ilionekana ukaribu wao si wa kikazi tu, kuna zaidi ya hapo kwa jinsi walivyoweka mambo yao.

Wiki moja kabla, Pamela alimkumbatia na kumbusu Liam kwenye shavu wakati wa onyesho la filamu hiyo jijini London, Uingereza.
Mwaka jana Liam aliulizwa kuhusu Pamela wakati wa utayarishaji wa filamu hiyo na kusema amependezwa sana naye. Anafaa sana kufanya naye kazi kutokana na tabia na haiba yake ya kuvutia.

"Siwezi hata kumaliza kumsifia, nitakuwa mkweli. Hana majivuno. Anaingia kazini na kufanya kazi. Ana ucheshi na ni mwepesi sana kufanya naye kazi. Atakuwa wa kipekee sana katika filamu hiyo," alisema Liam.

Pamela naye hakuwa nyuma kumsifia Liam, "Ni mwanaume kamili. Anakitoa kile kilicho bora ndani yako... kwa heshima, wema na fadhila kubwa. Ilikuwa heshima kubwa kufanya naye kazi."

Ingawa haijajulikana wazi ni lini Liam na Pamela walianza uhusiano wa kimapenzi, wawili hao wanaonekana kushibana sana. Wakati wa onyesho la filamu 'The Naked Gun' jijini New York, Marekani mnamo Julai 28, walipiga picha pamoja na watoto wao.

Pamela ana watoto wawili, Brandon, 29, na Dylan, 27, aliowapata na aliyekuwa mume wake Tommy Lee. Naye Liam ana watoto wawili pia, Micheál, 30, na Daniel, 28, aliowapata na marehemu mkewe Natasha.

Ikumbukwe Liam aliyewahi kuteuliwa kuwania Tuzo ya Oscar, alikutana na Natasha walipokuwa wakicheza tamthilia ya Anna Christie kwenye jukwaa la Broadway mwaka 1993, na kufikia Julai 3, 1994 wakafunga ndoa.

Machi 18, 2009, Natasha alifariki dunia baada ya kuumia kichwani katika ajali ya kuteleza kwenye barafu katika eneo la Mont Tremblant Resort, kaskazini-magharibi mwa Montreal. Liam alitoa viungo vya mwili wa mkewe kwa ajili ya wagonjwa waliokuwa wakihitaji baada ya kifo chake.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags