Rayvanny aliyetoa na kibao chake, Kwetu (2016), EP alizotoa ni Flowers (2020), New Chui (2021), Flowers II (2022), Unplugged Session (2022) na Flowers III (2023), huku albamu zikiwa ni Sound From Africa (2021) na The Big One (2024).
Ndiye mwanamuziki namba mbili anayefanya vizuri zaidi YouTube Afrika Mashariki, kwa ujumla video zake zimetazamwa zaidi ya mara bilioni 1.3 katika mtandao huo, na huko Boomplay nyimbo zake zimesikilizwa zaidi ya mara milioni 358.6.
Ni wazi kuwa mafanikio hayo yanatokana na idadi kubwa nyimbo alizonazo katika majukwaa hayo, ila wingi tu sio sababu bali ubora na mwendelezo mzuri wa kikazi vimechangia kwa kiasi kikubwa kuwa hapo alipo.
Ubora wa kazi zake umemwezesha kushinda tuzo kama Tanzania Music Awards (TMA) 2022, Zikomo Awards (Zambia) 2022, Afrimma (Marekani) 2022, EAEA Awards (Kenya) 2022, DIAFA Awards (Dubai) 2022 n.k.
Kabla ya hapo, tayari Rayvanny alikuwa ameshinda tuzo ya BET (Marekani) 2017 kama Viewer's Choice Best New International Act akiwa ni msanii wa pili Afrika Mashiriki baada ya Eddy Kenzo kutokea Uganda.
EP yake ya kwanza 'Flowers' ilitoka Februari 2020 ikiwa na nyimbo nane huku akiwashirikisha Messias, Mr. Blue na Malkia Karen. Hii ni EP iliyofanya vizuri hadi kuingia hatua ya kujadiliwa kwa ajili kuwania tuzo za Grammy.
Mnamo Februari 2021, akaachia albamu yake ya kwanza 'Sound From Africa' ikiwa na nyimbo 23 na kuwashirikisha wasanii zaidi ya 20 akiwemo Mbosso, Vanessa Mdee, Young Lunya, Innoss'B, Kizz Daniel, Jah Prayzah, Nasty C na Diamond Platnumz.
Albamu hii iliyotoka akiwa bado chini ya WCB Wasan, iiweка rekodi Afrika Mashariki kwa kusikilizwa zaidi ya mara milioni 100 ndani ya wiki moja pekee tangu itoke - zikiwa ni jumla ya data kutoka majukwaa yote ya kusikiliza muziki.

Mwaka 2022, Sound From Africa ilishinda tuzo kama Albamu Bora Afrika kutoka Zikomo Awards za nchini Zambia. Huu ni uthibitisho kuwa albamu hiyo ilikuwa kali na tangu wakati huo hajatoa nyingine zaidi ya kuwapa mashabiki wake EP.
EP yake ya pili 'New Chui' ilitoka Oktoba 2021 ikiwa na nyimbo sita na kumshirikisha msanii mmoja tu ambaye ni Abigail Chams aliyesikika katika wimbo, Stay.
Ni Abigail Chams yule ambaye alikuja kusaniwa Sony Music na miaka miwili baadaye akaandika rekodi kama mwanamuziki wa kwanza wa kike kutokea Afrika Mashariki kuchaguliwa kuwania tuzo za BET nchini Marekani.
EP ya tatu ya Rayvanny 'Flowers II' ilitoka Februari 2022 ikiwa na nyimbo tisa na kuwashirikisha wasanii watano ambao ni Roki, Nadia Mukami, Guchi, Ray C na Marioo. EP hii na ile ya mwanzo zilitoka Februari kwa ajili ya msimu wa wapendanao.
Baada ya kuachana rasmi na WCB Wasafi hapo Julai 2022, Rayvanny aliachia EP yake ya nne 'Unplugged Session' iliyotoka Novemba 2022 ikiwa na nyimbo nane. Hii ndio EP ya kwanza kutoka ikisimamiwa rasmi na rekodi lebo yake, NLM.
Kufikia Mei 2023, Rayvanny akaachia EP yake ya tano 'Flowers III' ikiwa na nyimbo tisa na kuwashirikisha wasanii wanne ambao ni Jay Melody, Bahati, Phina na Mac Voice ambaye aliwahi kumsaini NLM ila kwa sasa ameachana na lebo hiyo.
Albamu yake ya pili 'The Big One' ilitoka Novemba 2024 ikiwa na nyimbo 18 huku ikiwashirikisha mastaa kama Alikiba, Diamond, Harmonize, Marioo, Jay Melody, Phina, Yammi na Darassa, King Promise na Khalil Harisson.
Hivyo ukichukua nyimbo zote za EP na albamu alizotoa Rayvanny, zinafikia 83. Sio kazi rahisi hata kidogo, tuna wasanii wengi wamekuwapo kwenye muziki tangu mwanzoni mwa miaka ya 2000 na wamefanya vizuri na kutoa albamu lakini hawajaweza kurekodi idadi hiyo ya nyimbo.
Na kumbuka Rayvanny ana nyimbo nyingi tu tena maarufu ambazo hazipo katika albamu wala EP yoyote.
Huu ni uwezo wa juu zaidi upande wa utunzi, uthubutu na uwekezaji katika kipaji chake. Katika eneo hili, mwamba apewe maua yake sasa akiwahi hai ili aweze kuyanusa.
Leave a Reply