Mwanamuziki maarufu wa hip hop Busta Rhymes ametunukiwa rasmi nyota ya ‘Hollywood Walk of Fame’, ikiwa ni heshima kubwa kwa mchango wake katika muziki na burudani kwa ujumla.
Busta, ambaye jina lake halisi ni Trevor George Smith Jr., wakati wa kupokea tuzo hiyo ameleeza kuwa ilikuwa ni ndoto ambayo imetimia baada ya kutumikia tasnia ya muziki na burudani kwa zaidi ya miaka 30.
“Nimepitia mengi, lakini leo naona matunda ya kujituma, nidhamu, na upendo kutoka kwa mashabiki wangu duniani kote,” alisema Busta huku akishangiliwa.
Katika hafla hiyo, iliyofanyika jana Agosti Mosi, wasanii kama Spliff Star, Missy Elliott na Swizz Beatz waliungana na rapa huyo kwa lengo la kusheherekea mafanikio yake huku Elliott akimpongeza na kumpa maua yake akimtaja Busta kama ndio nguzo ya kweli ya Hip Hop ambaye ameacha alama isiyofutika.
Aidha kwa upande wa ‘Hollywood Walk of Fame’ wameeleza kuwa lengo la kumtunuku nyota hiyo ni kufuatia na mchango mkubwa katika muziki wa hip hop, uwezo wa kipekee wa uandishi na utumbuizaji, ushawishi wake katika kukuza na kuendeleza utamaduni wa hip hop pamoja na kuweka alama ya kudumu kwenye tasnia ya burudani, kupitia muziki na filamu.
Busta sasa anaungana na mastaa wengine waliotunukiwa heshima ya Hollywood Walk of Fame, akiwemo Snoop Dogg, Queen Latifah, Ice Cube, Diddy na wengineo.
Rapa huyo alianza safari yake ya muziki miaka ya 1990 akiwa na kundi la ‘Leaders of the New School’, kabla ya kuonesha ukubwa wake akiwa kama msanii wa kujitegea kwa kuachia hits kama Break Ya Neck, Touch It, na Put Your Hands Where My Eyes Could See.

Leave a Reply