Mwimbaji wa muziki wa Bongo Fleva, Juma Jux amesema katika vitu ambavyo hajawahi kujutia ni uamuzi wa kumuoa Priscilla Ajoke Ojo na kufunguka kuwa ana furaha ya kuwa na mke sahihi na kwamba hana mpango wa kuongeza wa pili.
Akizungumzia maisha ya ndoa, Jux alisema anashangaa kuona vijana wengi wanaogopa kuoa kwa kuhofia majukumu, lakini kitu ambacho hawakijui ni kwamba mbali na baraka za Mungu pia ndoa ina raha yake.
"Nashukuru nimepata mke sahihi, siwezi kumuolea mke wa pili licha ya kwamba dini inaruhusu, wito wangu ni vijana kuoa, wasihofie majukumu, ndoa ni tamu sana hasa pale unapompata mke sahihi," alisema Jux aliyefunga ndoa na mrembo huyo raia wa Nigeria Februari mwaka huu.
"Vijana wanaogopa sana kuoa siku hizi kwa kuhofia majukumu lakini ukweli ni kwamba mtoto wa kiume hutakiwi kuogopa wala kuyakimbia majukumu, ndio maana hata katika vitabu vya dini imeandikwa kwamba wanaume tutakula kwa jasho,"
Aliongeza Jux anayetamba na ngoma kadhaa ikiwamo Enjoy inayofanya vizuri sehemu mbalimbali, pamoja na Am Looking For You, Nisiulizwe, Sio Mbaya, Unaniweza na nyingine nyingine.
Kabla ya kufunga ndoa na Mnigeria huyo, Jux alishawahi kuhusishwa kutoka kimapenzi na Vanessa Mdee, Karen Bujulu, Nayika Thongom - raia wa Thailand, Jackie Cliff, Jacklyne Wolper na Mkenya Huddah Monroe.
Kwa sasa msanii huyo pia anatarajia kupata mtoto wa kiume na mke wake Priscy hii ni baaada ya mapema jana kuchapisha video ya sherehe ya kufichua jinsia ya mtoto wao.

Leave a Reply