Timu 5 duniani zilizocheza mechi nyingi za ligi bila kupoteza

Timu 5 duniani zilizocheza mechi nyingi za ligi bila kupoteza

Mabingwa wa kihistoria Tanzania, klabu ya Yanga imezuiwa kufikia rekodi ya kucheza michezo 50 mfululizo ya ligi kuu Tanzania bara bila kupoteza.

 

Ni klabu ya Ihefu, ambayo usingetarajia kuizuia Yanga, iliweza kufanya hivyo Jumanne hii (29.11.2022) katika uwanja wa Sokoine Mbeya baada ya kuichapa Yanga kwa mabao 2-1. Mara ya mwisho kwa Yanga kufungwa kabla ya mchezo wa Ihefu ilikuwa ni April 25,2021 dhidi ya Azam ilipolala kwa kufungwa kwa bao 1-0.

 

Hata hivyo michezo yake 49 kabla mchezo wa Ihefu iliyocheza bila kupoteza ni rekodi kwa Tanzania. Hakuna timu iliyowahi kufanya hivyo katika historia ya soka la nchi hiyo.

 

Kabla ya Yanga, Azam ndio iliyokuwa ikiishikilia rekodi ya kucheza michezo mingi bila kupoteza, wakicheza mechi 38, rekodi iliyodumu kwa muda wa miezi 18 kati ya Feb 23, 2013, hadi Oktoba 25, 2014

Rekodi ya Yanga kucheza michezo 49 bila kupoteza inafananishwa na rekodi ya washika mitutu wa London, Arsenal waliocheza michezo 49 bila kufungwa katika msimu 2003-2004.

 

Sasa sahau kuhusu rekodi ya timu ya wananchi Yanga na ile ya Arsenal, klabu hizi tano ziliwahi kucheza michezo  mingi zaidi ya ligi zao bila ya kupoteza na kuweka rekodi katika historia ya soka. 

 

  1. Al Ahly SC - Misri - 71

Al Ahly mabingwa wa kistoria wa Misri ni moja ya klabu kubwa na tishio barani Afrika, ikiwa na rekodi ya kutwaa mataji 42 ya ligi kuu ya nchini Misri na mataji 10 ya ligi ya mabingwa Afrika.

 

Ikiwa na makao yake katika jiji la Cairo klabu hii iliweka rekodi ya kucheza michezo 71 bila  kupoteza katika msimu wa mwaka 2004- 2007. Ikiwa ni sawa sawa na misimu mitatu rekodi hii haijavunjwa mpaka leo.

 

  1. Esperance Sportive de Tunis-Tunisia – 85

Esperance ni moja ya vilabu maarufu barani Afrika, ikianzishwa mwaka 1919 ni miongoni mwa vilabu vikongwe zaidi nchini Tunisia ikishabihishwa na jezi yake yenye mistari ya njano na  nyekundu,imefanikiwa kutwaa mataji 32  ligi kuu ya Tunisia na kimataifa ikiwa na jumla a mataji 13 yakiwemoa mataji 4 ya ligi ya mabingwa Afrika.

 

Esperance imewahi kucheza karibu  misimu ya ligi kuu Tunisia bila ya kupoteza ikicheza michezo  85 kati ya mwaka 1997 -2001. 

 

  1. Lincoln Red Imps Fc – Gibraltar – 88

Hawa ni mabingwa mara 24 wa ligi kuu ya  Gibraltar ikitumia uwanja wa Victoria, uwanja ambao unatumiwa na karibu timu zote kubwa zinazoshiriki ligi ya nchini humo.

 

Ukiacha kucheza michezo 88 ya ligi kuu bila ya kufungwa kati ya mwaka 2009 mpaka 2014 pia klabu hii inarekodi ya kutwaa mataji 14 ya ligi katika misimu 14 mfululizo kuanzia mwaka 2003 -2016.

Mwaka 2014 ilikuwa klabu ya kwanza kutoka Gibraltar kucheza ligi ya mabingwa barani Ulaya .

 

  1. FC Steaua Bucureşti - Romania - 106

FC Steaua Bucureşti ya Romania ni moja ya vilabu maarufu nchini humo, na ilifahamika zaidi katika soka la Ulaya baada ya kutwaa kombe la Ulaya mwaka 1986 ilipoichabanga Barcelona.

 

Ilikuwa haishikiki katika miaka ya 1980's. Iliwahi kucheza mechi 104 bila kufungwa kwa miaka zaidi ya minne kuanzia June 1986 mpaka Septemba 1989.

 

Katika kipindi hicho imefanikiwa kutwaa mataji manne ya ligi kuu. Inatajwa ndio klabu bora kuwahi kutokea Romania.

 

  1. ASEC Mimosa – Ivory Coast – 108

Arthur Pierre (katikati) wa Asec Mimosa akizingirwa na wachezaji wa Etoile Sportive du Sahel ya Tunisia, katika moja ya mechi za mabingwa Afrika, iliyopigwa Julai 24, 2005 kwenye uwanja wa Felix Houphouet Boigny mjini Abidjan 

Les Mimos, kama wanavyofahamika kwa jina la utani, ni moja ya vilabu vikongwe barani Afrika ikitwaa mataji 24 ya ligi kuu ya nchini Ivory Coast. Ikiwa na maskani yake Abidjan ina historia isiyozingatiwa sana ya kucheza michezo 108 ya ligi bila kupoteza. Ilifanya hivyo kati ya mwaka 1989-1994. Mpaka sasa rekodi yake haijawahi kuvunjwa.

ASEC ilizuiwa kuweka rekodi zaidi ya kutopoteza kwenye ligi kwa kuchapwa na wapinzani wao, klabu ya SO de l’Armée, ilikuwa mwaka 1994.

Kwa miaka 28 sasa, rekodi yake haijavunjwa na inabaki katika historia ya soka duniani ya kuwa timu iliyocheza michezo mingi zaidi ya ligi ya nyumbani bila kupoteza.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Saphinia Suleiman

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, career, skills development and technology.


Latest Post

Latest Tags