Mkuu wa Kitengo cha Sheria Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Christopher Kamugisha amesema wamesikiliza malalamiko ya pande zote mbili kuhusu wito wa wasanii Harmonize na Ibraah.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi za Basata Kamugisha amesema, Harmonize amewakilishwa na mwanasheria wake huku Ibraah akiwa na mwanasheria wake ambapo maamuzi waliyokubaliana ni kufika wote kwenye ofisi za Basata Jumatano Mei 14,2025 asubuhi saa 5 kwa ajili ya kusikilizwa.
"Tumefanikiwa kuongea na pande zote mbili, upande wa Harmonize na Ibraah, ila tumepanga kuongea siku ya Jumatano ili wasanii wote tuliowaita waweze kufika wakiwa na wanasheria wao.
"Harmonize hakufika leo amewakilishwa na mwanasheria wake na Ibraah alikuja na mwanasheria wake,"amesema Kamugisha ambaye hakusema walichozungumza kwenye kikao cha leo.
Utakumbuka Basata walitoa wito wa kuwaita wasanii Harmonize na Ibraah leo Jumatatu Mei 12, 2025. Ikiwa zimepita siku kadhaa tangu mwanamuziki wa Konde Gang inayomilikiwa na Harmonize, Ibraah kuweka wazi kuwa anataka kujitoa katika lebo hiyo lakini inamuwia ugumu kutokana na fidia anayotakiwa kulipa ambayo ni ya Sh1 bilioni.
Baada ya Ibraah uweka wazi hayo ikapelekea kuzuka kwa majibizano baina ya Ibraah na Harmonize. Hata hivyo jana Mei 11, 2025 lebo ya Konde Gang Music Worldwide ilitoa taarifa ya kumsimamisha Ibraa kutoa na kushiriki katika shughuli zozote za muziki hadi suala lake la kujitoa kwenye lebo hiyo litakapopatiwa ufumbuzi.
"Tungependa kufafanua kuwa machapisho na matamshi hayo siyo tu yanachafua taswira ya Lebo na wasanii wake, bali pia yanakiuka utamaduni wetu kama Watanzania na kukiuka masharti ya mkataba aliosaini na Lebo hii. Aidha, yanaenda kinyume na sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
"Kampuni yetu inahifadhi haki zake zote za kisheria katika suala hili. Wakati huu ambapo mchakato wa kushughulikia masuala haya unaendelea, umma unapaswa kufahamu kwamba Ibrah bado ni msanii halali wa Lebo ya Konde Gang Music Worldwide na ina haki ya kuendelea au kusitisha mkataba wake kwa kufuata na kuzingatia taratibu rasmi zilizowekwa katika mkataba aliosaini," imeeleza taarifa hiyo na kuongezea kuwa
"Konde Gang inampiga marufuku Ibraah dhidi ya kuchapisha, kutamka, au kufanya mawasiliano yoyote kuhusu suala hili kwenye vyombo vya habari au mitandao ya kijamii (kama vile Instagram, WhatsApp, Facebook, n.k.). Hii ni pamoja na mawasiliano ya aina yoyote ambayo yanaweza kuharibu taswira ya Lebo au kumdhalilisha mkurugenzi muwekezaji wa lebo ambaye ni msanii,"

Leave a Reply