Dar es Salaam. Je, umewahi kusikia siku ya muziki wa reggae duniani? Basi, siku hiyo ipo, ni leo. Siku hii huadhimishwa Julai Mosi ya kila mwaka ambapo ulimwengu unakumbuka na kufurahi pamoja kuhusu aina hiyo ya muziki.
Siku ya Kimataifa ya Reggae iliadhimishwa kwa mara ya kwanza mwaka 1994, na lilikuwa wazo la Andrea Davis, ambaye alipata msukumo wa kuianzisha baada ya kumsikia Winnie Mandela akitoa hotuba kuhusu matumaini na nguvu ambayo muziki huo uliwapatia raia wa Afrika Kusini wakati wa utawala wa ubaguzi wa rangi (apartheid).

Tangu kuanzishwa kwake, siku hiyo imekuwa ikiadhimishwa kila mwaka Julai Mosi, jijini Kingston, Jamaica.
Siku hiyo inalenga kusherehekea aina hii ya muziki iliyozaliwa katika nchi ndogo ya kisiwa katika ukanda wa Carribbean ambapo maelfu ya mashabiki na wanamuziki kote duniani hukusanyika kusherehekea historia ya kipekee ya reggae.
Tarehe hiyo ya tamasha ilipata umaarufu zaidi, baada ya kifo cha mwanamuziki mashuhuri wa reggae, Dennis Brown anayejulikana kama Mwana wa Kifalme wa Reggae aliyefariki Julai Mosi, 1999.
Wanamuziki mashuhuri wa aina hiyo ya muziki ni pamoja na Bob Marley “Mfalme wa Reggae” ambaye ndiyo kinara wa muziki huo duniani, akiwa ameacha urithi wa nyimbo nyingi zenye ladha, hisia na ari ya kuhamasisha ukombozi.
Mwanamuziki huyo alishiriki kikamilifu katika harakati za ukombozi wa bara la Afrika kupitia nyimbo zake ambazo ziliwaongezea Waafrika morali ya kupambana. Mwaka 1980, siku ya uhuru wa Zimbabwe, Bob Marley alikwenda kutoa burudani iliyoacha alama kubwa.
Nyimbo nyingi za Bob Marley zimekuwa zikitumika kwenye harakati za kisiasa ambapo wanasiasa wanaotaka kuleta mabadiliko wanatumia nyimbo hizo ili kuchochea ari na kasi ya kupambania mabadiliko.
Katika uchaguzi mkuu wa 2020, mgombea urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu alikuwa akitumia nyimbo za mwanamuziki huyo hususani “One Love” na “Africa unite” kabla ya kupanda jukwaani.
Nchini Kenya, pia, kiongozi wa ODM Kenya, Raila Odinga amekuwa akitumia nyimbo za Bob Marley kwenye kampeni zake za urais kwa kucheza na kuamsha ari ya wafuasi wake wanaojitokeza kwa maelfu kwenye mikutano yake.
Wanamuziki wengine wa reggae walioweka alama kwenye muziki huo ni pamoja na Peter Tosh, Bunny Wailer, Burning Spear, Toots Hibbert, Jimmy Cliff, and Lee "Scratch" Perry.
Wanamuziki wengine waliofanya mageuzi kwenye muziki huo barani Afrika ni Lucky Dube pamoja na Senzo, wote wakiwa raia wa Afrika. Wanamuziki hao walifariki kwa nyakati tofauti, lakini kazi zao zinaishi mpaka sasa.
Aina hiyo ya muziki ambao huchezwa kwa kurukaruka kwa mitindo tofauti, umekuwa kivutio kikubwa kwa watu wa rika zote kutokana na mahadhi yanayochezeka, ujumbe mzito na melodi ya kuvutia masikioni mwa wasikilizaji.
Leave a Reply