Kula kitimoto chanzo cha shinikizo la damu

Kula kitimoto chanzo cha shinikizo la damu

NYAMA ya nguruwe maarufu 'Kitimoto' imekuwa ikipendwa sana na watu wa mijini na vijijini licha ya kwamba bei yake ni ghali kuliko ya ng’ombe.

Kwenye baa mbalimbali za jiji la Dar es Salaam nyama hii inauzwa kiasi cha Sh.12, 000 kwa kilo na kwa mikoani ikiuzwa kati ya Sh. 6000 au 5000 kwa kilo.

Hata hivyo nyama hii imewekwa katika kundi la nyama nyekundu ambayo inadaiwa kuwa ni hatari na ina madhara makubwa kiafya kuliko ulaji wa nyama nyeupe.

Kwa wasiofahamu nyama nyekundu ni ile ambayo ina rangi nyekundu kabla ya kupikwa mfano nguruwe mwenyewe, ng’ombe, mbuzi, na wanyama wote wanaotembea kwa miguu minne.

Aidha nyama nyeupe ni zile ambazo zina rangi nyeupe kabla ya kupikwa mfano kuku, bata, samaki, mbuni na wanyama wote wanaotembea kwa miguu miwili.

Hebu basi leo tuangalie madhara ya nyama ya nguruwe kama anavyotufahamisha Walbert Mgeni Ofisa Lishe, Mtafiti, Elimu na Mafunzo ya Lishe kutoa Taasisi ya Tiba na Lishe.

Mgeni anasema nyama hiyo ya nguruwe ina kitu kinaitwa lehemu kitaalamu cholesterol, ambayo hukaa kwenye mishipa ya damu ya binadamu na kusababisha damu kushindwa kupita vizuri.

“Hii husababisha viungo muhimu vya mwili kama moyo kukosa damu ya kutosha na kuanza kushindwa kufanya kazi. Japokua cholesterol ni muhimu kwenye mwili wa binadamu lakini inayotengenezwa na mwili inatosha hii inayoongezeka kutoka kwenye nyama ni hatari sana.

“Tena nifafanue kuwa mafuta yanayotokana na kitimoto yanaganda  na mtu akiyala yanaenda kuganda ndani ya mwili hasa kwenye mishipa ya damu hivyo kipenyo cha mshipa kinapungua na  kufanya moyo kufanya kazi kubwa katika kusukuma damu ndio maana unakuta mtu anapata  shindikizo la juu la damu, kupooza viungo au vifo vya ghafla,” anasema

Anasema ulaji wa nyama hiyo mara kwa mara usababisha moyo kuchoka na ndio maana wanasisitiza kuwa sio vizuri watu kutumia na kuongeza kuwa hata nyama za mbuzi ni mbaya kwani uwafanya watu kuumwa magoti.

Mgeni anasisitiza kwamba nyama nzuri ambayo watu wanashauliwa kula ni ile nyeupe ambayo ni kuku, samaki, dagaa na jamii ya ndege.

“Tunashauri watu wapendelee kula zadi nyama nyeupe na sio nyekundu. Ulaji wa nyama yoyote yenye mafuta inauwezo mkubwa wa kuleta matatizo katika mishipa ya damu kwa sababu inaongeza rehemu kubwa katika mwili,” anasema.

Anasema madhara mengine ya ulaji wa nyama nyekundu ni kupata unene uliopitiliza.

“Nyama nyekundu ina kiwango kikubwa cha mafuta ambacho watu wengi hula kama yalivyo, mfano kwenye nyama ya nguruwe, mafuta haya usababisha unene na kitambi ambavyo ni hatari sana kwana uleta matatizo mengi ya kiafya na kisaikolojia, vifo vya ghafla pia vikiwa hatari zaidi kwenye swala la unene,” anasema.

Mgeni anasema kwa kuwa nyama pia ina faida katika miili yetu basi nyama nyeupe ni salama sana kuliko nyekundu.

“Nyama ya nyeupe yaani samaki, kuku, bata na ndege wengine wanaoruhusiwa kuliwa ni salama sana kuliko nyama nyekundu kama mbuzi, ng’ombe, nguruwe na wengine ni hatari sana. 

“Na kama wewe tayari una tazizo la moyo, presha, kisukari na kansa huu ni wakati sahihi wa kuacha kula nyama nyekundu kabisa kwani zinaweza kukuletea matatizo makubwa zaidi,” anasema

Naye Happy Welema mkazi wa Buza jijini Dar es Salaam, anasema ni muhimu jamii ikazingatia maelekezo ya wataalamu wa afya hasa ya   kaucha kula nyama hizo nyekundu.

“Kila siku tunaelezwa kuwa nyama hizi nyekundu kwa afya zetu si nzuri hivyo basi hatuna budi kuziacha na kula nyama nyingine tunazoshauriwa ili kuepuka maradhi,” anasema.

Aidha anasema sasa hivi kumekuwa na ongezeko la vifo vya ghafla na hiyo yote ni kutokana na ulaji wa vyakula ambavyo si salama kwa afya zao.

“Unakuta kila siku mtu anakula nyama choma na bia, yaani ni mlo mmoja tu ambao una mafuta lazima tu katika hali ya kawaida utapata maradhi kama shindikizo la damu.

“Mimi na familia yangu tumebadlisha kabisa mtindo wetu wa kula, tumekuwa tukizingatia maelekezo ya wataalamu wa afya tena kwa kuacha kabisa ulaji wa nyama nyekundu,” anasema.

Aidha Happy ameiomba Serikali chini ya Wizara husika ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kujipanga kutoa elimu kwa jamii juu ya umuhimu wa kula nyama nyeupe na si nyekundu.

Vilevile wanadda huyo ameitaka jamii kutambua kuwa nyama tunazokula siku hizi sio halisi tena.

“Kwani ukiangaliwa nyama ya kuku inayoliwa sana katika baadhi ya hoteli kuwa zinadaiwa kuwa zinawekwa kemikali nyingi ambazo ni hatari kwa mwili wa binadamu,” anasema.

 






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Detricia Pamba

A Digital Journalist, Content Creation Executive at Mwananchi Communications Ltd and Chief Editor of Mwananchi Scoop. I'm also writes stories around Technology, every Wednesday on Mwananchi Scoop. My other famous segments on Mwananchi Scoop include LISTI and WHO’S HOT.


Latest Post