Kinachomtofautisha Chege na wengine

Kinachomtofautisha Chege na wengine

Mkali wa Bongo Fleva kutoka TMK Wanaume Family, Chege kwa miaka zaidi ya 20 ametengeneza nyimbo nyingi kubwa ndani ya kundi hilo na akiwa pekee yake akifanya kazi na wasanii wa ndani na kimataifa.

Hakuna ubishi Chege Chigunda ni miongoni mwa wasanii wachache wa Bongo Fleva wenye mwendelezo mzuri wa kufanya vizuri tangu wametoka, wengi alioanza nao kwa sasa hawasikiki kabisa. Fahamu zaidi.

Jina alilopewa na wazazi wake ni Said Juma Hassan, hilo la Chege amelitoa katika kitabu cha The River Between (I995) alichokisoma shule na kuvutia na uhusika wa mtu aliyetumia jina hilo katika kitabu hicho kilichoandikwa na Ngugi wa Thiong’o kutokea Kenya.

Chege alianza muziki na kundi la TMK Wanaume Family mwaka 2002 lakini umaarufu wake ulikuja baada ya kuachia wimbo wake ‘Twenzetu’ akiwa na Mh. Temba, Ferooz na YP, kisha ukafuata ‘Lover Boy’, nyimbo hizi zilifanya vizuri kuanzia mwaka 2003.

Aliyekuwa Mtangazaji wa Clouds FM, Marehemu Gardner G. Habash ndiye aliyesimamia wimbo huo wa Chege ‘Twenzetu’ tangu unaandikwa hadi kurekodiwa studio za MJ Records chini ya Miikka Mwamba kutokea Finland.

Utakumbuka Mikka Mwamba ambaye alifanya kazi FM studio kati ya mwaka 1999 hadi 2004, wimbo wa Dully Sykes ‘Julieta’ ndio ulimtambulisha katika Bongo Fleva, kisha zikafuata nyingine kama Mama Yangu (Banana Zoro) na Tamala (Hardmad).

Pia kuna Nakupenda Mpenzi/ Tentemente (Dudu Baya), Eno Maiki (Ziggy Dee), Babygal (Mad Ice), Kamanda (Daz Nundaz), Kwenye Chati (Balozi Dola Soul), Mkiwa (K Sal), Elimu Mitaani.com & Kitu Gani (D Knob), Maria Salome (Saida Karoli), n.k.

Kuna mambo mawili ambayo Chege hawezi kuyasahau katika safari yake ya muziki, mosi; ni kuvunjika kwa kundi la TMK Wanaume Family, pili; kurushiwa makopo jukwaani katika shindano la ‘Nani Mkali’ walipokuwa wakichuana na TMK Wanaume Halisi.

Unaambiwa wimbo wa mwisho kwa Chege kuandika katika karatasi ni ‘Dar Mpaka Moro’ ambao aliuandika akiwa safarini, tangu hapo amekuwa akiandika tu nyimbo zake studio mara baada ya kusikia mdundo na kuvutiwa nao, basi anashuka nao tu.

Na huo ndiyo ulikuwa wimbo wa kwanza kuwapa Chege na Mhe. Temba mafanikio makubwa kimuziki kwani ulipelekea wasanii hao kusafiri kwa mara ya kwanza kwenda Dubai na Uingereza kufanya shoo iliyowalipa vizuri.

Je, wajua kuwa Chege anashirikisha sana wasanii wa kike katika nyimbo zake?, ameshafanya kazi na Malaika (Uswazi Take Away), Vanessa Mdee (Manjegeka), Nandy (Kilele cha Chura), Ray C (Najiuliza), Saida Karoli (Kaitaba), Phina (Sinsima), Rosa Ree (Boss) n.k.

Sasa baada ya kushirikishwa na Chege katika wimbo, Uswazi Take Away (2014) ndipo Malaika alivuma kimuziki, na wawili hao walikutana kwa Director Adam Juma na Malaika alikuwa akifanya kazi kama mpambaji (makeup artist) kwa wakati huo.

Ikumbukwe Malaika ndiye msanii wa kwanza wa kike Tanzania kutoka kwenye Bongo Fleva kufanya muziki aina ya Mchiriku, ni baada ya kutoa wimbo wake, Mwantumu (2014) ambao aliwashirikisha Chande na Tin White.

Video ya wimbo wa Chege, Waache Waoane (2016) akimshirikisha Diamond Platnumz ndio ya kwanza kwake kutazamwa (views) zaidi ya mara milioni 1 YouTube, hiyo ni sawa na Fid Q kupitia video ya ngoma yake, Fresh Remix (2017) akimshirikisha Diamond pia.

Muunganiko wa Chege na Mhe. Temba kimuziki uliokuja na nyimbo kali ulianza baada ya muuza kanda (tape) maarufu za wasanii wakati huo, Mamu Store kumshauri Mkubwa Fella kuwa Chege na Temba wafanye kazi pamoja maana kazi zao zinauzika sana.

Ni Mh. Temba aliyepitia makundi ya muziki kama BWV (Brothers with Voice), baadaye akiwa sekondari mwaka 1998 akajiunga na Scrimmage, kisha mwaka 2001 akiwa na Daz Baba wakaanzisha Nduli Mobb, mwaka 2005 akajiunga na TMK Wanaume Family.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Christina Lucas


Latest Post

Latest Tags