MIAKA MITATU YA UKIMYA WA KOFFEE
Ni miaka mitatu sasa imepita mashabiki wa muziki hawajapokea kazi yoyote kutoka kwa mkali Koffee ambaye ni mwimbaji, rapa na mpiga gitaa kutokea Jamaica.
Kazi yake ya mwisho kuachia ilikuwa ni Albamu ya 'Gifted' iliyotoka Machi 25, 2022 yenye jumla ya nyimbo kumi ambazo ni pamoja na x10, Defend, Shine, Gifted, Lonely na nyinginezo.
Mwaka 2019 aliandika historia baada ya kuachia Ep yake ya 'Rapture' nyenye nyimbo tano ambazo kati ya hizo mbili ni za reggae. Ep hiyo ilishinda Tuzo za Grammy 2020 katika kipengele cha Albamu Bora ya Reggae na kumfanya kuweka rekodi ya kuwa msanii mwenye umri mdogo zaidi kushinda katika kipengele hicho. Ep hiyo pia ilifanikiwa kuingia kwenye Top 10 ya albamu kali Ulaya.
Miongoni mwa ngoma kali zinazopatikana kwenye Ep hiyo iliyoshinda Grammy 2020 ni pamoja na 'Toast' ilishinda Wimbo Bora wa Mwaka kwenye Tuzo za The Jamaica Music Industry Association's.
"Toast" ni miongoni mwa nyimbo za mwanzo za Koffee, ilitoka mwaka 2018 ikitayarishwa na Walshy Fire na 'izybeats' wa Major Lazer. Kwenye video wimbo huo anaonekana msanii Chronixx na Protoje.
Koffee aliendelea kufanya vizuri kwenye anga za kimataifa kwani kabla ya kufikisha miaka 20 tayari alikuwa na kolabo na rapa wakubwa Marekani akiwemo Gunna ambaye walishirikiana kwenye wimbo wa 'W' lakini pia mwaka 2019, rapa wa Canada Tory Lanez alitengeneza remix ya wimbo wa "Toast" ikiwa ni kuonesha kukubali uwezo wa msanii huyo.
Mwaka 2020, Jarida la Elle lilimtaja Koffee kati ya wanawake 10 wanaofuatiliwa zaidi na ambao wanaweza kubadilisha wakati ujao. Wengine waliotajwa kwenye orodha hiyo ni pamoja na Mowalola Ogunlesi, Tobi Kyeremateng, Ngozi Onwurah, Simi Lindgren, Balanda Atis, Magdalene Abraha, Holly Fischer, Celeste na Margaretsby.
Hata hivyo, msanii huyo amekuwa kimya kwa kipindi kirefu kitu ambacho kimepelekea maswali mengi kwa wafuatiliaji wa muziki wake, lakini taarifa nzuri ni kwamba Koffee ameahidi kuachia album yake mpya mwaka huu.
Akizungumza kwenye mahojiano aliyofanya kwenye Tamasha la Reggae Land lililofanyika nchini Uingereza 2024 aliweka wazi ujio wa album hiyo ambayo hakuitaja jina lakini alisema ina collabo motomoto.
"Nina albamu mpya itakayotoka hivi karibuni," aliiambia Reggae Interviews.

Leave a Reply