Kwa miaka ya hivi karibuni muziki wa Singeli umechukua nafasi kwenye tasnia ya burudani nchini, ambapo wasanii wa Bongo Fleva wameonesha kukubali kuwa kwa sasa muziki huo ni alama ya kuwatambulisha katika soko la muziki kimataifa.
Jitihada za wadau wa muziki wa Singeli kuupeleka kimataifa zimefanyika kwa kipindi cha muda mrefu huku zikitokea kampeni kama Singeli 2 the World kwa ajili ya kusapoti na kuufikisha muziki huo katika soko la dunia.
Licha ya hayo kwa upande wa msanii wa Bongo Fleva, Alikiba inaonekana kuwa tofauti kwani hadi sasa hajawahi kufanya aina hiyo ya muziki. Licha ya kuwa kwenye nafasi nzuri na kupigiwa kampeni.
Baadhi ya wasanii wakubwa tayari wameachia ngoma ambazo zipo katika mahadhi ya Singeli na kupokelewa kwa ukubwa akiwemo Diamond Platnumz, ambaye Februari 2, 2025 aliachia wimbo 'Nitafanyaje' ukiwa katika mtindo huo, wimbo huo ulipokelewa vizuri kwenye majukwaa ya kusikilizia nyimbo kama YouTube ambapo umefanikiwa kutazamwa zaidi ya mara laki tano.
Aidha, Harmonize ni moja kati ya wasanii ambao walianza kuusapoti muziki wa Singeli miaka mitano iliyopita baada ya kuachia mkwaju wake 'Hujanikomoa' uliotoka Februari 8, 2020. Ukipata mapokezi makubwa kwenye majukwaa mbalimbali kama YouTube ambapo video yake imetazamwa zaidi ya mara milioni 3.1.
Konde hakuishia hapo aliachia tena ngoma nyingine iliyoitwa 'Kamaliza' inayopatikana katika albamu yake ya pili High School, katika wimbo huo kamshirikisha msanii wa Singeli Sholo Mwamba.
Mwaka 2020, msanii wa Bongo Fleva nchini, Rayvanny alishirikiana na Mfalme wa Singeli Dulla Makabila katika ngoma ya Miss Buza ikiwa katika mahadhi ya Singeli. Wimbo huo ulipokelewa kwa ukubwa kwenye majukwaa ya muziki kama YouTube ambapo umetazamwa zaidi ya mara milioni 15.
Hakuishia hapo miaka miwili iliyopita Rayvanny alipiga remix ya ngoma ya Kitu Kizito ya kwake Dj wa muziki Singeli, Misso Misondo ngoma ambayo video yake iliachiwa Desemba 5,2023, mpaka sasa imetazamwa zaidi ya mara milioni 6.5 YouTube.
Pia, kwa upande wa msanii wa Bongo Fleva kutoka lebo ya WCB Wasafi, Zuchu mwaka 2021 akiwa na mwaka mmoja tangu kusainiwa katika lebo hiyo aliachia ngoma yake 'Nyumba Ndogo' ikiwa katika mahadhi ya Singeli na kupokelewa kwa ukubwa kwenye majukwaa ya muziki, video yake ikitazamwa zaidi ya mara milioni 40 Youtube.
Zuchu ameendelea na muziki wa Singeli hata mwaka 2024, aliachia wimbo 'Hujanizidi' akiwa na D Voice wimbo ambao unapatikana katika albamu yake ya Peace and Money ya 2024.
Hata hivyo, Zuchu ameendelea kuunga mkono muziki huo kwa kuwashika wasanii wachanga ambao wachipukia katika muziki wa Singeli akiwemo Dogo Paten na kushirikiana katika wimbo wake Afande.
Remix iliyopata mapokezi makubwa kwenye mitandao ya kijamii hata mtaani na kuupa hadhi muziki wa Singeli. Zuchu anakwambia kwa upande wake haijawahi kuwa ngumu kuufanya muziki huo kwani unaendana na muziki wa Taarab ambao amekua akiusikia kwenye familia yake.
Aidha, usiku wa kuamkia leo Mei 20, 2025, msanii wa Bongo Fleva, Jux amewashtua mashabiki wa muziki baada ya kuchapisha kipande cha wimbo wake wa Singeli EX wa Nani kutoka kwenye Ep ya 'A Day To Remember' inayotarajiwa kutoka hivi karibuni.
Wasanii wengine wakubwa kutoka katika kiwanda cha Bongo Fleva ambao tayari wameshiriki kufanya muziki wa Singeli ni pamoja na Marioo akiwa na ngoma kama (Nakuja Remix aliyoshirikishwa na Balaa Mc 2020.
Nimegonga remix aliyoshirikishwa na Kayumba 2021, Tunamjua kutoka kwenye albamu yake ya The Kid You Know ya 2022, Lavalava (Wanga akiwa na Meja Kunta ya 2020).
Ibraah kupitia ngoma kama (Do Lemi Go akiwa na Kinata Mc 2021, Wivu Remix 2024 akiwa na Dj Mushizo, Jay Combat na Baddest 47, Kwani We Nani aliyoshirikishwa na Meja Kunta) na wengine wengi.

Leave a Reply