Peter Akaro
Baada ya rapa aliyetamba na kundi la Nako 2 Nako Soldiers na sasa Weusi, Lord Eyes kudai muziki wa Hip Hop Bongo kuna sehemu umekwama, wasanii wenzie wamejibu kauli hiyo.
Lord Eyes alisema muziki wa Hip Hop Bongo unarudi nyuma kutokana na kutopewa nafasi kubwa kama waimbaji, fursa wanazopewa ni chache mno.
"Kama gemu ya Hip Hop ukiangalia kitaalamu kabisa imerudi nyuma, ukifuatilia kwa kuanzia kwa kina Professor Jay, Jay Moe, Solo Thang mpaka kuja kina Chid Benzi, Fid Q, Joh Makini, Lord Eyes na Nako 2 Nako, ukilingaanisha na sasa utaona imerudi nyuma," amesema.
"Kwa hiyo hilo ni jukumu la wana-hip hop wote kuhakikisha tunarudi kule tulipokuwa mwanzo, ni wazi kama tasnia tunaona muziki unarudi nyuma badala ya kwenda mbele, kwa hiyo hilo ni jukumu la watu wote kusimamia na kukaa pamoja," amesema Lord Eyes.
Akizungumzia hilo Kalapina wa Kikosi cha Mizinga amesema sio kweli Hip Hop imekwama bali ni wasanii wenyewe wa muziki huo kukubali hali hiyo na kukimbilia aina nyingine za muziki kama Amapiano.
"Sio kweli, watu waendelee kutunga zile kazi ambazo zilikuwa zinavuma na kutamba kwa sababu huu ni muziki wa kuelimisha, sasa watu wameacha misingi hiyo ndio inapelekea kuonekana hivyo ila watetezi wa Hip Hop bado wapo," amesema.
Ameendelea kusema "Leo hii hao kina (Lord Eyes) wameingia hadi kwenye Amapiano, muziki ambao naona kama wa upotoshaji kwa sababu ni muziki ambao mwanaume hawezi kucheza hadi ajilegezelegeze,"
Kwa upande wake P Mawage (P The MC) amesema baadhi ya wasanii wa Hip Hop waliotangulia ndio wanafanya muziki huo kukwama kutokana na mtindo wao kazi ila Hip Hop bado ipo sana tu.
"Sasa imekuwa rahisi msanii mkongwe aliyeheshimika kwenye Hip Hop kuachana na muziki huo na kuimba vitu vingine kwa sababu walishakubaliana na hali hiyo, na sisi ambao tunapingana na hilo tunaokana tuna chuki," amesema P Mawenge.
"Leo hii Lord Eyes ametoa Amapiano ila mimi nikimuuliza kwanini unaimba Amapiano na wewe ndio kioo kwetu tunakuangalia kama kaka kwenye Hip Hop, ataniona kama na chuki ila akikaa kwenye vyombo vya habari anasema Hip Hop imekwamba, sio kweli," amesema.
Amesema wakati wanaanzisha Tamaduni Muziki mwanzo mwa 2010 walipata mapokezi makubwa hadi nje ambapo wasanii kama kina Khaligraph Jones wa Kenya walikuwa wanawaunga mkono, ila kwa ndani wasanii wakubwa wa Hip Hop hawakuwa na moyo huo, hivyo wao kudai Hip Hop inakwama wao pia wanahusika kuikwamisha.

Leave a Reply