Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imeanzisha mpango wa kusaidia wasanii wanaokabiliwa na uraibu wa dawa za kulevya, lengo likiwa ni kuwasaidia kupona na kurudi katika harakati zao.
Akizungumza jijini Dar es Salaam Machi 19,2025 Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, alitangaza kuwa mpango huo utaanza na msanii wa hip-hop, Rashid Makwiro maarufu kama Chid Benzi, ambaye atakuwa balozi kwa wasanii wenzake wanaopambana na uraibu wa dawa za kulevya.
"Tunaanza naye na endapo atafanikiwa kupona, tutaendeleza mpango huu kwa wengine wanaohitaji msaada. Msanii huyo atawekwa chini ya uangalizi maalum ili kusaidia katika safari yake ya kupona,”alisema Lyimo
DCEA pia imeshirikiana na Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) kuhakikisha wasanii wanakaa mbali na dawa za kulevya na kuzuia utayarishaji wa muziki unaohamasisha matumizi ya dawa hizo.
Ili kuimarisha mpango huu, mamlaka hiyo itashirikisha wasanii maarufu katika kampeni za uhamasishaji, wakitumia majukwaa ya burudani kuelimisha umma kuhusu madhara ya dawa za kulevya.
Mbali na kuwasaidia wasanii, DCEA imetenga zaidi ya Sh 800 milioni kwa ajili ya kujenga kituo cha tiba kwa ajili ya waathirika wa dawa za kulevya huko Itega, Dodoma.
Kituo hicho, ambacho kwa sasa kiko katika hatua za ujenzi, kitatoa mafunzo ya stadi za maisha kwa wale wanaopata nafuu kutokana na uraibu wa dawa za kulevya.
Wahitimu wa mafunzo hayo watapatiwa vifaa vya kuanzia biashara zao ili kuwasaidia kurejea katika jamii na kujikimu kimaisha.
“Wale watakaomaliza hatua za ukarabati watapewa ujuzi wa kazi na pia vifaa vya kuanzisha shughuli zao za kujitegemea. Baadhi yao pia watapewa ajira ndogo ndogo katika kituo hicho,” aliongeza Lyimo
Aidha, watu wanaopenda kupata mafunzo ya ufundi katika taasisi kama Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta) watapewa msaada chini ya mpango huu.
DCEA pia itasaidia waathirika wa zamani wa dawa za kulevya kupata mikopo ya serikali, ambapo asilimia 10 ya fedha zinazopatikana na zitatengwa kwa ajili yao. Mpango huu utaanza kutekelezwa katika mikoa ya Arusha, Dodoma, na Tanga.

Leave a Reply