Huu wimbo umemtia Diamond hasara tu!

Huu wimbo umemtia Diamond hasara tu!

Huu wimbo umemtia Diamond hasara tu!

Staa wa Bongofleva kutokea WCB Wasafi, Diamomd Platnumz ameshirikiana na wasanii wengi wa kimataifa ambao wameikuza na kuitangaza chapa yake na sasa ni miongoni mwa wasanii wenye nguvu ya ushawishi barani Afrika.

Diamomd aliyetoka kimuziki mwaka 2009 ameshirikiana na wasanii wakubwa na maarufu kama Alicia Keys, Ne-Yo, Rick Ross, Omario, Davido, Patoranking, Morgan Heritage, Mr. Flavour, Rema, P Square, Koffi Olomide n.k.

Utakumbuka kolabo yake na Davido wa Nigeria, My Number Remix (2013) ndio ya kwanza kumtangaza kimataifa ambapo kwa mara ya kwanza aliwania tuzo za MTV MAMA (2014) kama Msanii Bora wa Kiume na Wimbo Bora wa Kushirikiana.

Hata hivyo, kuna kazi ambazo alifanya na wasanii wa kimataifa na baadaye kugeuka shubiri kwake, miongoni mwa hizo ni 'Hallelujah' kutoka kwenye albamu yake ya tatu, A Boy From Tandale (2018) iliyozinduliwa Nairobi, Kenya.

Wimbo huo alishirikisha kundi la muziki wa Reggae kutokea Jamaica, Morgan Heritage ambalo lilianzishwa mwaka 1994 na watoto watano wa msanii wa Reggae Jamaica, Denroy Morgan.

Mwaka 2016 Morgan Heritage kupitia albamu yao, Strictly Roots (2015) walishinda tuzo yao ya kwanza ya Grammy kwenye kipengele cha Albamu Bora ya Reggae, kisha wakaja kushinda tuzo hiyo kwa mara ya pili mwaka 2019 kupitia albamu yao, Avrakedabra.

Diamond kufanya kazi na Morgan Heritage ilikuja baada kuachia ngoma yake na Ne-Yo, Marry You (2017) iliyokuwa inasubiriwa tangu walipokutana kwenye tuzo za MTV Africa Music Awards Kwazulu-Natal-2015 (MAMA) huko Durban, Afrika Kusini.

Basi video ya Hallelujah ikatoka na kuweka rekodi ya kupata 'views' zaidi ya milioni 1 YouTube ndani ya saa 15 na kuvunja rekodi iliyokuwa inashikiliwa na Wizkid wa Nigeria kupitia wimbo wake, Closer uliyopata 'views' milioni 1 ndani saa 23.

Vilevile wimbo huo uliweza kushika namba moja kwenye chati za BBC Radio 1Xtra za nchini Uingereza kupitia kipindi chao cha Afro Boss, ikizipita nyimbo kama Inde wa Heavy K, Maradona wa Niniola n.k.

Kufanya vizuri kwa wimbo huo, kulipelekea kundi la Morgan Heritage kufanya kazi na wasanii wengine wa Afrika kama Stonebwoy (Ghana), Harmonize (Tanzania), Patoranking (Nigeria) na Jose Chameleon (Uganda).

Lakini kama nilivyoeleza hapo awali kuwa wimbo huo uligeuka shubiri kwa Diamond, ni kutokana kwa sasa hawezi kuutumbuiza popote pale wala sura yake haiwezi kuwa na furaha ikitazama video yake, sababu ni kama ifuatavyo.

Mosi, ni pale Februari 2018 ambapo Baraza la Sanaa Taifa (Basata) walipotuma majina ya nyimbo 15 kwenda Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), majina hayo ni ya nyimbo ambazo zilipaswa kufungiwa kutokana kukiuka maadili.

Wimbo wa Diamond, Hallelujah ulikuwa ni miongoni mwa nyimbo hizo, TCRA iliviagiza vyombo vya habari kusitisha kuzicheza kutokana na kuwa na maudhui ambayo ni kinyume na maadili na huduma za utangazaji.

Kutokana na hilo, huo ukawa mwanzo wa wimbo huo kupotea kwenye vituo vya redio na televisheni na sasa Diamond hawezi kuuimba kwenye jukwaa lolote lile kwani atakuwa anavunja sheria, na hajawahi kufanya hivyo tangu wakati huo.

Ikumbukwe wimbo mwingine wa Diamond, 'Waka' ambao kamshirikisha Rick Ross kutokea Marekani nao ulifungiwa kipindi hicho na tangu hapo hajaachia wimbo wowote akimshirikisha msanii kutoka nchini humo.

Pili, ukitazama video ya Hallelujah iliyofanyika nchini Uingereza na kuongozwa na Director Moe Musa, utawaona Rich Mavoko na Harmonize kuanzia 'verse' ya pili hadi ya tatu, wawili hawa walikuwa marafiki na baadaye kugombana.

Utakumbuka mwishoni mwa mwaka 2019 Harmonize aliamua kuondoka WCB Wasafi yake Diamond akiwa ni msanii wa pili kufanya hivyo baada ya Rich Mavoko ambaye alidumu hapo tangu Machi 2016 hadi Julai 2018.

Kwenye jukwaa la Wasafi Festival mwaka 2019, Diamond alieleza kwa hisia kali kusalitiwa na mtu wake wa karibuni aitwaye 'Jeshi', ni Harmonize aliyekuwa na mkataba wa miaka 10 na WCB Wasafi ila akaondoka akiwa ameutumikia takribani miaka minne tu.

Kwa muktadha huo, Diamond anawaona wawili hao ni kama wasaliti kwake baada ya kuachana na WCB Wasafi, ni vigumu sana kuona tabasamu usoni mwake wakati akitazama video ya wimbo, Hallelujah uliotengenezwa na Prodyuza Laizer.

Tatu, video ya wimbo, Hallelujah haijafanya vizuri sana YouTube kama kolabo zake nyingi za kimataifa, ikiwa na miaka saba tangu itoke ndio kwanza ina 'views' milioni 15, imeachwa hadi nyimbo za kawaida kama Naanzaje, Baba Lao n.k.

Kumbuka hiyo ni video iliyoigharamikia sana, imefanyika nje ya Tanzania na Director wa nje pia, ila kuna nyimbo kama Waah! ft. Koffi Olomide, imefanyika Tanzania na Director wa Tanzanzia, Kenny ila imefanya vizuri. Ndani ya miaka minne tu imefikisha 'views' milioni 168 ikishika nafasi ya pili kati orodha ya video za Diamond zilizotazamwa zaidi.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Masoud Kofii


Latest Post

Latest Tags