Mtindo wa kusimulia visa na matukio kupitia muziki hasa wa Rap au Hip Hip uliteka hisia za wengi kipindi cha nyuma, jumbe za kuelimisha ndizo zilichukua nafasi kwa asilimia kubwa tofauti na sasa.
Ni vigumu kusahau ngoma kama; Bosi ya Ferooz, Barua ya Daz Nundaz, Nikusaidieje ya Profesa Jay, Stori Tatu ya Jay Moe, Mkuki Moyoni ya Afande Sele na Elimu Dunia ya Daz Baba.
Hata hivyo, kizazi kipya cha muziki huo nacho kimekuwa kikifanya aina hiyo ya muziki, ila mabadiliko katika tasnia na aina yao ya uandishi, vinatajwa kupelekea kutofika mbali zaidi licha ya kazi hizo kupendwa na wengi. Miongoni mwa walioweza kufanya hivyo ni pamoja na;
1. P Mawenge (P The MC) - Huna Jipya
Kwa mujibu wa Profesa Jay, huyu ndiye Rapa bora kwake kwa kizazi hiki ambaye anaona ana uwezo mzuri wa kusimulia (storyteller) jambo na likaeleweka na wengi, kitu ambacho P Mawenge anasema anajivunia.
Albamu yake 'Mwingi wa Habari' imejaa simulizi za kutosha, nyimbo kama Huna Jipya, Baba Msaliti, Mama Mjane ni mfano halisi, na hata EP yake, Simu na Matukio, kaonyesha ufundi na ustadi wa kusimulia.
"Ukaleta michongo ya kuirubuni bajeti, unapika ndondo ili uwende saloni ukaseti," P Mawenge katika wimbo wake 'Huna Jipya' akielezea kisa cha dada wa kazi aliyekuja kubadili tabia nyumbani kwao na kuwa mtu mwingine kabisa!.
2. Dizasta Vina - Shahidi
Sio Rapa tu, bali ni mshahiri mzuri ambaye hachoshi ukimsikiliza, ana utajiri mkubwa wa maudhui unaomtofautisha na wasanii wengi wa sasa, ngoma zake kama; Sister, Konda na Shahidi ni uthibitisho kuwa anaweza kazi.
"Viongozi hawakubebwa na vyeo vyao maana wote walikuwa mbali na ridhaa, niliona kofia za Ufalme zikielea kando yao ila hakuna aliyekuwa hai kuzivaa" Dizasta katika wimbo wake, Shahidi akielezea kisa cha meli kuzama kwa uzembe.
"Niliwapa taarifa lakini wakanitwika maudhi, waliishia kulia na hazikusikika sauti, walipambana mwisho yaliwafika mauti, nilibaki hai nikiziandika sarufi," Dizasta anamalizia.
3. Nikki Mbishi - Kijusi
Katika albamu yake ya kwanza 'Sauti ya Jogoo' amefanya kazi kubwa sana kiuandishi, ina visa vilivyoshiba, ngoma kama; Nyakati za Mashaka, Play Boy, Kijusi, Malimwengu na Nimezama ni kazi bora kuwahi kutokea.
"Mashtaka bila hatia je wanapaswa kutuhumiwa?, mimi ndio Kijusi niliyenyimwa haki ya kuzaliwa...... Mama mlinde Kijusi ili Nabii azaliwe, jamii inamhitaji hivyo mimba ithaminiwe," Sehemu ya wimbo wa Nikki Mbishi, Kijusi akijivika uhusika wa mimba iliyotolewa ambayo sasa inazungumza.
4. Songa - Usiku
Mtindo wake wa kusimulizia unaambatana na burudani, licha ya kukupa elimu lakini anakuacha na tabasamu, amefanya hivyo kwenye nyimbo zake kama; Usiku, Picha na Kikosi cha Mizinga.
"Mara akaanza kulia eti Kaka una roho ngapi, nikamwambia usilie mimi ndio Songa nina roho safi," Songa katika ngoma yake 'Usiku' akisimulia tukio la kumuokoa dada aliyekuwa anajiuza kutokana na ugumu wa maisha katika mikono ya wabakaji.
5. Stereo - Rafiki
Albamu yake ya kwanza, African Son chini ya M Lab (Music Laboratory), Stereo amesimulia visa vingi kupitia nyimbo zake kama; Afande Nyati, Rafiki, Salamu Kutoka Jela na The Life.
"Maisha yake hayaendi poa aliyemtamani amemtapeli, mimba alifanikiwa kuitoa ila UKIMWI amefeli," Stereo katika wimbo wake, Rafiki akieleza kisa cha binti aliyeharibiwa maisha na kiongozi wa dini.
Nikki Mbishi, P Mawenge, Songa wafunguka
Akizungumza na Mwananchi, Nikki Mbishi amesema tatizo lililopo kwenye uandishi wa stori za sasa katika muziki ni kwamba wasanii wengi hawajachimba vitu sana na hawana taarifa za kutosha.
"Mfano Rapcha anaweza kusikiliza Zali la Mentali ya Profesa Jay akawa anaipenda ile stori, lakini stori za Rapcha anaweza kumsikilizisha Profesa Jay akaona anahadithia tu watoto wa rika lake ambazo wanazipenda," amesema Nikki Mbishi.
Kuhusu kwanini wao wameshindwa kutoa nyimbo kubwa kama 'Zali la Mentali', Nikki amesema tupo kwenye zama ambazo watu hawasikilizi muziki, watu wamekuwa wavivu, anapenda nyimbo starehe tu kama Amapiano.
"DJ anakuambia utoe wimbo una dakika mbili na nusu ili aweze kufanya 'mixing' ila Timberlake akitoa wimbo una dakika nane watu wanaujua, ila huku DJ anapiga kiitikio tu, sasa mtu kaandika stori yake watu wataijua vipi?, bora upige nyimbo tano zilizokamilika kuliko nyimbo 20 vipande vipande," amesema Nikki.
Naye P Mawenge amesema nyimbo za simulizi zinapendwa sana mitaani ila kwenye majukwaa bado kutokana watu huko wanapenda muziki wa kuchezeka sana.
"Kwenye haya mambo kuna vitu vitatu; kuna mtu anaweza kuandika vizuri ila kusimulia hanogi, kuna anasimulia vizuri ila anaandika vibaya, halafu kuna mtu ni bora kwenye vyote," amesema P Mawenge.
Kuhusu kauli ya Profesa Jay kwake, P Mawenge amesema aliipokea kama tuzo na imemtanulia biashara kwake; kama kuna mtu alikuwa anataka kuandikiwa stori ni rahisi kumchagua kwa sababu Profesa Jay amesema.
Kwa upande wake Songa amesema nyimbo za simulizi za wakati huu hazikai muda mrefu maana wasanii wengi wamejikita kuburudisha kuliko kuelimisha.
"Kila muziki unaosikia ni wa kiburudani tu, umeimbwa vitu hivi vya mapenzi, kwa kifupi stori nyingi zinawekwa za mapenzi kuliko stori za maisha yanayoendelea mtaani kila siku, mimi nimekuwa nikijaribu kuweka elimu na burudani," amesema Songa.
Songa anasema wasanii wa zamani kama Wagosi wa Kaya walikuwa wanaelemisha zaidi lakini burudani unaipa humo humo ndani ya elimu na siku zote elimu ndio inaishi muda mrefu zaidi kuliko burudani ambayo ni kitu cha muda mfupi.
Leave a Reply