WANAWAKE WANAPOYAEGEMEZA MAISHA YAO MITANDAONI

WANAWAKE WANAPOYAEGEMEZA MAISHA YAO MITANDAONI

Wengi wetu huwa tunapitia mitandao ya kijamii hususan facebook au Instagram.

Huenda katika kupitia kwetu huko tukawa tumekutana na ukurasa wa mwanamke mrembo hasa ambaye anatuvutia kwa bashasha zake kutokana yale anayoyaweka katika ukurasa wake.

Unaweza kukuta ni mwanamke mwenye elimu nzuri na kazi nzuri yenye kipato cha kuridhisha kinachomuwezesha kuishi maisha ya hali ya juu.

Ukurasa wake kuanzia asubuhi mpaka jioni unakuwa unapambwa na mapichapicha yake akionekana katika maeneo tofauti tofauti kuanzia anapoamka asubuhi anapofanya mazoezi, awapo ofisini, anapohudhuria vikao kikazi, anapopata mlo wa mchana na pale anapokuwa na mitoko ya jioni.

Unapomfuatilia unagundua kwamba hajawahi kuwepo katika sehemu moja zaidi ya mara mbili.

Ni mtu wa kubadilisha viwanja anapokuwa na mitoko ya jioni au mitoko ya mwishoni mwa wiki. Mavazi yake ni ghali na mwili wake unavutia kama wa mwana mitindo jambo ambalo linamfanya kuwa na mashabiki wengi wanaomfuatilia kwenye ukurasa wake zaidi ya milioni moja.

Kila akiweka picha kinachofuatia ni likes na comments za wafuasi wake hususan wanaume wakimsifu kwa jinsi alivyo mrembo na anavyopendeza huku wengine wakijitokeza kumuomba namba yake ya simu ili kuwa na ukaribu naye lakini kwa bahati mbaya hakuna aliyebahatika kupata namba yake ya simu na hata wale wanaume waliokuwa wakimfuata chemba kwenye ukurasa wake hakuwa akiwajibu.

Unapojaribu kumchunguza unagundua kuwa mrembo huyu hakuwa na ukaribu na mtu yeyote katika maisha yake ya kawaida na si wanaume pekee bali pia hata wanawake wenzie kutokana na matukio mengi kuonekana akiwa peke yake ukiacha yale matukio ya mikutano yake ya kikazi anayoyaweka kwenye ukurasa wake mara chache.

Unabaki kujiuliza huyu ni mwanamke wa aina gani?

Iwapo ikitokea mrembo huyu hajaweka chochote kwenye ukurasa wake wengi hujiuliza ni jambo gani limempata mrembo huyu maridhawa.

Likizo za mrembo huyu ni za kutalii katika nchi mbalimbali duniani tena akifikia katika hoteli kubwa kubwa za nyota tano na mitoko yake ni ile ya kwenye mighahawa mikubwa na ghali.

Kwa fikra za kawaida unaweza kudhani ni mwanamke mwenye furaha kupindukia na hata ukatamani aina ya maisha anayoishi. Unajikuta ukitamani kila kitu kinachomhusu na hata kutaka kuiga aina ya maisha anayoishi lakini huna uwezo wa kipato cha kukuwezesha kuishi aina ya maisha anayoishi.

Lakini ghafla ukurasa wake unakumbwa na ukimya jambo ambalo linawashtua wafuasi wake na baada ya kufuatilia inakuja kujulikana kwamba mrembo yule amefariki kwa kujiuwa huku sababu ikiwa haijulikani. Jambo hilo linawashtua wengi. Inakuwaje mrembo kama yule mwenye karibu kila kitu binadamu anachokitamani afikie hatua ya kukatisha uhai wake kikatili.

Naam hivi ndivyo tulivyo, kuvutiwa na kutamani aina ya maisha wanayoishi baadhi ya wenzetu katika mitandao ya kijamii bila kujua undani wao, yaani kile walicho nacho ndani ya mioyo yao.

Je mnadhani ni jambo gani linaweza kuwa limempata mrembo huyu?

Jambo ambalo wengi tunaweza kuwa hatukulijua ambalo lilikuwa likimsumbua binti huyu ni utupu aliokuwa nao ndani yake. Kwa nje alikuwa na furaha lakini kwa ndani alikuwa ana sonona iliyokuwa ikimsumbua kwa muda mrefu.

Hakuwa na ukaribu na mtu yeyote kutokana na kujitenga na jamii iliyomzunguka kwa muda mrefu ikafikia kumuacha kama alivyo akaamua kuitafuta kupitia mitandao ya kijamii lakini pia haikuweza kuziba pengo hilo.

Hali hiyo ilimletea sonona lakini aliendelea kuificha. Alikuwa akionyesha furaha kwenye mitandao wakati alikuwa ana huzuni, alikuwa anaonekana kucheka wakati anatamani kulia, alikuwa anaonekana mwenye amani moyoni wakati alikuwa akiumia ndani ya moyo wake hadi akafikia kukatisha uhai wake kwa kukosa msaada.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Shaban Kaluse

A Sales and Marketing in the hospitality Industry and also a freelance journalist, writing about love and relationships and educative articles which aims for youths, every Tuesday on Mwananchi Scoop.


Latest Post

Latest Tags