Safari ya siku 19,154 za maisha ya mwanahabari Sharon Sauwa imehitimishwa leo kufuatia maziko yake yaliyofanyika katika Makaburi ya familia nyumbani kwao Pugu Mwakanga jijini Dar Salaam.
Sharon aliyekuwa mwandishi wa habari wa kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL) akiripoti kutoka mkoani Dodoma, alifariki dunia alfajiri ya Agosti 19,2025 wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kufutia kuugua kwa takribani wiki mbili.
Mamia ya waombolezaji walioungana katika misa ya maziko iliyofanyika katika kanisa la Mtakatifu Francis Pugu wameeleza kuwa tasnia ya habari imepata pigo kufuatia kifo cha mwanahabari huyo aliyetajwa kuwa na weledi wa hali ya juu katika utekelezaji wa majukumu yake.
Akitoa salamu zake Waziri wa Mawasiliano, Habari na Teknolojia Jerry Silaa amemtaja Sharon kama miongoni mwa waandishi mahiri waliofanya kazi zao kwa weledi.

Amesema katika kipindi chote alichokiwa bungeni Sharon alionesha umahiri mkubwa katika kuripoti habari za bunge na kuwa daraja kati ya wananchi na Serikali.
“Kila mbunge au aliyewahi kuwa mbunge angepata nafasi ya kusema angesema namna alivyokuwa rafiki, ndugu na mama. Alikuwa mwandishi mwenye weledi, akiwa na jambo atakuuliza kwa unyenyekevu. Nitoe pole kwa tasnia ya habari,”amesema Silaa ambaye pia alitoa salamu za pole kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo Profesa Palamagamba Kabudi.
Akitoa salamu za rambirambi Mkurugenzi Mtendaji wa MCL Rosalynn Mndolwa-Mworia amemtaja Sharon kama alikuwa mlezi wa waandishi wengi wa habari ndani na nje ya kampuni hiyo.
“Katika kipindi chote cha miaka 13, Sharon alikuwa mwalimu kwa wenzie, tangu kutokea kifo chake salamu tulizozipata zimedhihirisha aliishi vyema na wenzie. Leo tumejumuika kumsindikiza katika safari yake ya mwisho tukimuombea afike salama tukijua ipo siku tutakutana,” amesema Rosalynn
Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali mstaafu Ludovick Utoh amemtaja Sharon kama mwandishi makini aliyekuwa akiandika kile anachokiamini bila kupindisha ukweli.
“Alikuwa mwandishi anayeandika kitu anachoamini, alielimisha Watanzania wengi.Kilichotokea kwa Sharon ni wakati wake umefika, tuendelee kumuombea kwa Mungu kwa sababu ana haki ya kuvuna shambani kwake,” amesema Utoh
Mbunge mstaafu Joseph Selasini amesema hakuna mwanasiasa ambaye hajaguswa na maisha ya Sharon kwani alitumia kalamu yake vyema katika kuripoti habari za siasa na bunge.
“Hakuna mwanasiasa ambaye hakuguswa na Sharon, alifanya kazi kubwa ya kufundisha na kuelimisha Taifa hili. Leo tunamshukuru Mungu kwa zawadi ya maisha yake.
Alikuwa mama na dada mwema akishirikiana na watu wote. Alikuwa mshauri mzuri, huwezi kumuona akiwa na uchungu hata akiwa na tatizo kubwa kiasi gani,” amesema Selasini ambaye pia ni jirani wa wazazi wa Sharon.
“Alifuata tabia za wazazi wake kupenda kusali, niwakumbushe waandishi wa habari Sharon alishawahi kupata kesi kwa sababu ya kazi yake lakini sijui iliisha namna gani. Nilikuwa nakutana naye ananiambia kaka usisahau kuniombea twende tukasali. Ama kwa hakika tunapaswa kila siku kuandaa vifo vyetu, hakuna kifo cha ghafla,”.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, Meneja wa Dawasa Ukonga, Mhandisi Honest Makoyi amesema licha ya Sharon kuwa rafiki na dada kwa waziri huyo alikuwa mtu wake wa karibu katika kazi.
Mwakilishi wa Klabu ya waandishi wa habari Dodoma (Dodoma Press Club)
Mussa Yusufu amesema Sharon amekuwa katika klabu hiyo kwa takribani miaka 15.
Amemwelezea kama mwandishi mwenye kipaji cha pekee, ambaye licha ya kipaji chake aliwashirikisha wengi waliopata wasaa wa kukutana naye.
"Alizichakata kwa weledi habari za Bunge la Tanzania kwa weledi, tunafahamu zilikiwa ngumu lakini alizichakata kwa umahiri na kuweza kueleweka na wananchi wa kawaida.
"Sharon hakuwa mwalimu pekee bali alikuwa mama wa kutupatia fursa na mawazo chanya sisi vijana kuhusu kazi na maisha," amesema Mussa.
Wasifu
Sharon alizaliwa Machi 10, 1973 na safari yake ya elimu alipita katika shule mbalimbali jijini Dar es Salam kabla ya kujiunga na chuo cha uandishi wa habari.
Mwaka 2002 alihitimu diploma ya uandishi wa habari na kuanza kazi kama mwandishi katika kampuni ya The Guardian Limited akiandikia gazeti la Nipashe kabla ya mwaka 2013 kujiunga na kampuni ya Mwananchi Communications Ltd.
Leave a Reply