Saratani ya shingo ya kizazi

Saratani ya shingo ya kizazi

Mambo vipi msomaji wa jarida lako pendwa la Mwananchi Scoop? Leo makala yetu inazungumzia saratani ya shingo ya kizazi ikiwa ni mwezi Januari, mwezi ambao shirika la afya duniani limeuchagua kuwa mwezi wa kuifahamisha jamii kuhusiana na ugonjwa huu ili kumlinda mtoto wa kike.  

SHINGO YA KIZAZI NI NINI?

Shingo ya kizazi ‘cervix’ ni sehemu ya kizazi kati ya uke na mji wa mimba. Sehemu hii ina kazi nyingi ikiwemo;

  • Kupitisha mbegu za kiume kuelekea katika mji wa uzazi na hatimaye mirija ya uzazi ili kupevusha yai,
  • Kupitisha damu ya hedhi
  • Mlango anaopitia mtoto wakati wa kuzaliwa. 

SARATANI YA SHINGO YA KIZAZI NINI?

Saratani ya shingo ya kizazi ni saratani inayotokea katika sehemu ya shingo ya kizazi ambapo seli za kansa hujiunda na kusababisha kizazi kupata madhara katika afya ya uzazi.  Saratani ya shingo ya kizazi husumbua wanawake dunia nzima na ni kansa inayoonekana na kusababisha vifo vya wanawake wengi zaidi katika nchi zinazoendelea, wale wasiopata fursa ya kuchukua vipimo vya afya ya shingo za kizazi kitaalamu (Pap testing) au kupewa chanjo dhidi ya human papillomaviruses (HPVs).

Sataratani ya shingo ya kizazi hutofautiana sana na saratani nyingine za kwenye mfuko wa uzazi kama kansa ya uterus au endometrial cancer. Kansa hii ikigundulika mapema ina uwezekano mkubwa sana wa kupona. Chanjo dhidi ya HPVs, virusi wanaosadikika kuleta saratani ya shingo ya kizazi ni hatua madhubuti ya kuzuia ugonjwa huu.

 

TAKWIMU

Saratani ya shingo ya kizazi ndiyo saratani inayoongoza kwa kusababisha vifo vya wanawake wengi duniani. Inakadiriwa kuwa asilimia 85 ya vifo hivi hutokea katika nchi zinazoendelea. Kwa Tanzania, wastani wa wanawake 6,241 huugua saratani hii kila mwaka, ambapo 4,355 kati yao hufa, hii ni kwa mujibu wa ripoti ya shirika la afya duniani (W.H.O) ya mwaka 2010.

Saratani ya shingo ya kizazi ndio saratani ya kwanza kwa wanawake nchini Tanzania na Saratani namba moja kwa wanawake walio kati ya umri wa miaka 15 hadi 44 ambao wako kwenye hatari kubwa ya kupata saratani hii.

AINA ZA SARATANI YA SHINGO YA KIZAZI.

Kuna aina mbili za seli kwenye shingo ya kizazi (cervix) ambazo ni squamous cell carcinoma na glandular cell carcinoma.  Jambo muhimu la kufahamu ni kwamba saratani inapoanza huwa ni vigumu sana kuigundua kwani haioneshi dalili zozote, hivo unaweza usigundue mpaka pale saratani imefikia hatua mbaya zaidi. Seli za kansa ya shingo ya kizazi hukua taratibu na huchukua miaka michache kwa seli za kawaida kubadilika kuwa seli za kansa, ndio maana inashauriwa kufanya vipimo mara kwa mara ili kugundua mapema.

CHANZO CHA SARATANI YA SHINGO YA KIZAZI

Ni nini chanzo cha saratani ya shingo ya kizazi?

 Karibu saratani zote za shingo ya kizazi husababishwa na maambukizi ya muda mrefu ya moja ya virusi wa aina ya HPVs.

Maabukizi ya HPV ni ya kawaida na watu wengi walioambukizwa HPV hawapati saratani ya shingo ya kizazi. Kuna aina tofauti za HPV zaidi ya 100 na baadhi ya aina chache ndiyo wanaohusishwa na saratani ya shingo ya kizazi. 

Virusi hawa HPV huambukizwa kupitia ngono au kwa kugusana ngozi. Utafiti unaonyesha kuwa watu wengi huambukizwa virusi hawa katika kipindi fulani cha maisha yao. Mambukizi haya kwa kawaida hupona yenyewe. Kwa baadhi ya wanawake, maambukizi haya huendelea kudumu na kuanza kuleta mabadiliko kwenye seli za shingo ya kizazi. Mabadiliko haya huweza kugundulika kwa kuchukua vipimo vya mara kwa mara – Pap testing.

Wanawake wengi wanaopata ugonjwa huu huwa na kisababishi kimoja au zaidi kinachojulikana ambacho huongeza hatari ya kuupata. Vifuatavyo ni baadhi ya vyanzo vya saratani ya shingo ya kizazi:-

  • Kuanza vitendo vya ngono katika umri mdogo (chini ya miaka 16)
  • Kuwa na mahusiano ya kimwili na zaidi ya mwanaume mmoja
  • Maambukizo ya virusi vya HPV (Human papilloma virus)
  • Umri zaidi ya miaka 30
  • Upungufu wa kinga mwilini (VVU/UKIMWI)
  • Uvutaji wa sigara
  • Kupata mimba katika umri mdogo
  • Kuzaa mara kwa mara
  • Kuwa na mahusiano ya kimwili na mwanaume ambaye mwenza wake ni muathirika wa saratani ya shingo ya kizazi.
  • Kuwa na mahusiano ya kimwili na mwanaume ambaye hajatahiriwa
  • Historia ya saratani ya shingo ya kizazi katika familia

 

DALILI NA VIASHIRIA VYA KUWA NA SARATANI YA SHINGO YA KIZAZI.

Saratani ya shingo ya kizazi katika hatua za awali haina dalili au viashiria vyovyote. Ila pale saratani itakaposambaa huonesha dalili zifuatazo:-

  • Kutokwa na damu katika uke ambayo sio ya kawaida. Damu hii inaweza kuwa matone, au damu inayotoka katikati ya mzunguko wa hedhi.
  • Kutokwa na damu baada ya kujamiana baada ya tendo la ndoa.
  • Maumivu wakati wa kujamiana.
  • Kutokwa na majimaji ukeni kusiko kawaida yenye harufu na maumivu ya tumbo chini ya kitovu.
  • Kupungua kwa hamu ya kula
  • Kupungua uzito
  • Kuhisi uchovu
  • Maumivu kwenye mgongo, mguu na nyonga.

HATUA ZA SARATANI YA SHINGO YA KIZAZI.

Hatua za saratani ya shingo ya kizazi ni kielelezo cha namna saratani hiyo ilivyosambaa ndani ya mwili wa mgonjwa siku alipofanyiwa uchunguzi. Kujua hatua ya ugonjwa huu ni muhimu katika kuamua aina bora ya tiba ya kumpa mgonjwa huyu. Hatua ya saratani ya shingo ya kizazi huamuliwa kwa kutazama kiwango cha uvimbe, usaambaaji kwenye lymph nodes, na usambaaji kwenye sehemu nyingine za mwili.

Saratani ya shingo ya kizazi imepangwa katika hatua kuanzia 0 hadi IV, hatua hizo ni pamoja na:-

. Stage 0: Hatua hii si ya kansa inayoshambulia. Seli ambazo si za kawaida bado zipo kwenye ngozi ya juu ya shingo ya kizazi.

 

. Stage I: Kuna kiwango kidogo cha uvimbe ambao bado haujaanza kusambaa kwenye lymph nodes au sehemu zingine.

 

. Stage II: Saratani imesambaa nje ya shingo ya kizazi na mfuko wa uzazi lakini bado haijashambulia kuta za pelvis au sehemu za chini mfano uke.

 

. Stage III: Saratani imesambaa hadi kufikia maeneo ya chini ya uke na kuta za pelvis. Uvimbe unaweza kuwa unaziba ureters (mirija ya kutiririsha mkojo kutoka kwenye figo hadi kibofu cha mkojo). Kansa bado haijasambaa kwenye sehemu nyingine za mwili.

 

. Stage IV: Hii ni hatua juu kabisa ya ugonjwa huu, hatua ambapo saratani imesambaa hadi kwenye kibofu cha mkojo au sehemu ya haja kubwa au kwenye maeneo mengine ya mwili.

KINGA NA TIBA YA SARATANI YA SHINGO YA KIZAZI.

Tiba ya saratani ya shingo ya kizazi hutegemea na hatua ya ugonjwa husika. Baadhi ya matibabu ni kama:-

Upasuaji

Kufanyiwa upasuaji huhusisha kuondoa mfuko wa mimba (uterus) na viungo vingine vilivyoathirika kama ovari na mirija ya uzazi

Chemotherapy

Matibabu kwa kutumia dawa kali ambayo huangamiza seli za saratani ili kuongeza muda wa kuishi.

Mionzi.

Matibabu kwa njia ya mionzi ili kuua seli za saratani pale ambapo upasuaji inaonekana kuwa changamoto au kama kuna uhitaji wa kuangamiza seli lengwa za saratani.

Pia, mwanamke anaweza kuzingatia yafuatayo kujilinda na saratani ya shingo ya kizazi.

  • uchunguzi wa kitabibu

Kila mara wanawake wanashauriwa kutembelea vituo vya afya ili kujua hali za afya zao.

Kupata chanjo dhidi ya virusi vya HPV. Hii itasaidia endapo mtu ameambukizwa, kinga ya mwili itapambana na vijidudu hivo. Pata HPV vaccine (hii yashauriwa kati ya umri wa miaka 12 hadi 26 chini ya mwongozo wa daktari)

  • Elimu Kwa jamii.

Jamii inapaswa kuelimishwa kuhusu ugonjwa huu namna ya kujilinda na namna ya kukabiliana nao endapo mtu ameambukizwa.

  • Mtindo wa maisha.

Kujiepusha na mitindoo hatarishi ya kimaisha kama ngono zembe na uvutaji wa sigara inayosababisha kuupata ugonjwa huu ni jambo la kuzingatia

  • Pap testing

 Waweza kupata Pap test mara 1 kwa mwaka au mara 1 kwa miaka 2- 3, hii itategemea ushauri wa daktari,umri,hali yako ya afya kwa ujumla, na majibu uliyoyapata katika vipimo vilivopita.  

  • Tumia kinga (condoms)

 Hii husaidia kupunguza maambukizi ya magojwa ya zinaa.

  • Kula chakula chenye afya hasa vyakula asilia
  • Kunyonyesha kunapunguza hatari kwa mwanamke kuugua saratani
  • Epuka matumizi ya dawa za uzazi wa mpango zenye madhara
  • Kufanya mazoezi ya mwili mara kwa mara.

Ugunduzi wa mapema katika hatua za awali za ugonjwa huu na kupatiwa matibabu stahiki na kwa wakati.

Imeandaliwa na Mark Lewis






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Detricia Pamba

A Digital Journalist, Content Creation Executive at Mwananchi Communications Ltd and Chief Editor of Mwananchi Scoop. I'm also writes stories around Technology, every Wednesday on Mwananchi Scoop. My other famous segments on Mwananchi Scoop include LISTI and WHO’S HOT.


Latest Post

Latest Tags