Peter Akaro
Mgogoro wa hivi karibuni kati ya Diamond Platnumz na Willy Paul wa Kenya uliotokea katika tamasha la Furaha City nchini humo, ni matokeo ya mlundikano wa mambo mengi ya muda mrefu dhidi ya staa huyo wa Bongofleva.
Willy Paul alihusishwa kuvuruga mpangilio wa show hiyo kwa kile anachodai kupigania usawa kwa wasanii wa Kenya dhidi ya wageni kitu kilichosababisha Diamond kushindwa kutumbuiza na kuondoka.
Hata hivyo, hii sio mara ya kwanza kwa Willy kuonyesha ana ishu dhidi ya Diamond licha ya hapo awali kumtaja kama mtu anayemvutia (role model) hadi kujiita Willy Paul Msafi katika mitandao ya kijamii.
Akiwa tayari amefanya kazi na wasanii wa Bongofleva kama Harmonize, Nandy na Rayvanny, ni wazi ishu ya Willy kwa Diamond inachangiwa na kutokukamilika kwa kolabo yao ambayo ilirekodiwa miaka 10 iliyopita.
Ndoto yake kubwa ilikuwa ni kutoa wimbo na Diamond na alipambania sana hilo kwa muda mrefu lakini baada ya kushindikana akaonekana kuingia kinyongo dhidi ya Diamond ikiwa ni pamoja na kumshambulia katika mitandao.
Februari 19, 2023, Willy aliibuka mtandaoni na kudai kuchukizwa na kauli ya Diamond aliyesema kuwa yupo single kufuatia kuachana na Zuchu, hivyo wao ni kama kaka na dada tu na sio kama ambavyo watu walivyokuwa wakidhani.
“Sasa umepiga kiki zimeisha unaanza kuzirudia, waaah earth is hard, stori za kawaida hizo bwana au Zuu (Zuchu) amefanya ile kitu? Mimi nilishaacha sasa hivi ni muziki tu my friend,” aliandika Willy Paul kupitia Insta Story.
Tukirudi nyuma hadi mwaka 2013 wakati akiwa anafanya muziki wa Injili, Willy alisema ndoto yake ni kuja kufanya kazi na Diamond kwa sababu ndiye aliyemvutia kuingia katika muziki tangu akiwa kijana mdogo kabisa.
Ni kauli iliyoacha maswali kwa mashabiki wengi kwa sababu ni mara chache sana kumsikia msanii wa Injili kutaka kufanya kazi na msanii wa muziki wa kidunia (secular artist) ila Willy Paul hakujali hilo, alichotaka ni kolabo na Diamond.
Na mwaka uliofuata akajipa jina la Msafi, tangu mwaka 2014 amekuwa akijiita ‘Willy Paul Msafi’ katika muziki wake na hata kwenye mitandao wa kijamii, imekuwa ndio chapa yake rasmi!
Haikuchukua muda akaonekana studio na Diamond pamoja na mtangazaji wa Citizen Radio, Willy M Tuva, Willy alithibitisha kuwa wamesharekodi kazi yao na muda wowote mashabiki wataisikia, kubwa zaidi ndoto yake inaenda kutimia.
“Najisikia vizuri sana, imekuwa ni ndoto come true, Diamond ni role model wangu, nilipata interest ya Bongofleva nikiwa mchanga sana, tangu hapo nikaanza kuimba kwa kuiga wasanii wa Bongo, nilimkubali sana Diamond,” alisema Willy Paul.
Kipindi hicho Willy alikuwa ameshaachia nyimbo zake kama ‘Sitolia’ na ‘Lala Salama’, na ikumbukwe Diamond pia ana wimbo unaitwa ‘Lala Salama’ ambao ndio umebeba jina la albamu yake ya pili iliyotoka mwaka 2012, hivyo utaona kwa kiasi gani alimkubali Mondi.
Hata Diamond alipofungua ofisi yake ya kwanza ya WCB Wasafi iliyokuwa Sinza, Dar es Salaam, Willy alimtembelea hapo Machi 2017 na walipiga picha pamoja na ikatarajiwa siku za usoni ile kazi yao itatoka ila haikuwa hivyo kitu kilichozaa kinyongo.
Ila licha ya kolabo yao kutokamilika, Diamond alitoa nafasi kwa wasanii wake, Harmonize na Rayvnany waliokuwa bado chini ya WCB Wasafi kufanya kazi na Willy ambapo waliachia nyimbo, Pilipili (2018) na Mmmh (2019).
Katika tamasha hilo, DJ alipocheza kolabo yake na Rayvanny, Mmmh (2019), Willy akiwa jukwaani aliuita wimbo huo takataka na kumtaka DJ aachane nao kwani hawezi kuutumbuiza!
Hivyo, ni wazi Willy ana ishu zake binafsi dhidi ya Diamond na watu wake karibu na sio kama anavyodai kupigania maslahi ya wasanii wa Kenya. Unapiganiaje maslahi ya tasnia yako kwa kukashifu wasanii waliokuinua kimuziki wakati hakuna anayekujua?
Mwaka 2017 nilikutana na Willy pande za Msasani, Dar es Salaam, wakati huo alikuwa amekuja Tanzania kufanya ziara katika vyombo vya habari nchini ili kutangaza kazi zake na kutafuta fursa ya kufanya kazi na wasanii wa hapa.
Kiukweli alikuwa bado anajifuta sio tu kwa Tanzania bali hata kwao Kenya, hivyo kwa kuwa wasanii wa Tanzania wanafanya vizuri zaidi Kenya, aliamini kufanya kazi na wasanii wa Bongo itakuwa rahisi kwa yeye kukubalika kwao.
Diamond ambaye tayari alishakuwa msanii mkubwa Afrika akishinda tuzo mbili za MTV Europe Music Awards (EMAs), pengine aliona bado ni mapema kufanya kazi na Willy ila akampa kina Rayvanny na Harmonize, kazi ambazo zilimpa sifa kubwa kwao.
Cha ajabu mtu huyo leo hii anakuwa sehemu ya mvutano uliofanya Diamond asitumbuize kwa madai amependelewa na waandaaji wa tamasha, hata kama hilo lina ukweli, Diamond kamzidi Willy kila kitu ndio maana alitambulishwa kama mtumbuizaji mkuu katika tamasha hilo.
Kwa kifupi Willy Paul anapaswa kujiangalia tabia zake, ni hivi majuzi tu katoka kumuomba msamaha mwanamuziki mwenzake wa Kenya, Bahati baada ya kudai alitembea na mke wa Bahati, Diana Marua, madai ambayo amekuja kukiri hayakuwa na ukweli wowote.
Leave a Reply