Nitapataje kazi bila kushikwa mkono

Nitapataje kazi bila kushikwa mkono

Ngoja leo tuambizane ukweli hapa mpambanaji wangu. Je, ni kipi unafikiria baada ya kumaliza masomo yako? Je, kauli hii inatembea kichwani mwako au umeamua kujitambua na kufanya kile ambacho kinawezekana kulingana na wakati tulionao?

Hizi ni kauli za vijana wetu wasomi waliomaliza elimu ya juu.

Katika karne hii ya 21 bado tuna vijana wanaamini kwamba baada ya kumaliza Chuo na kufaulu ni ngumu kupata kazi mpaka ushikwe Mkono. Yaani atokee mtu akuwezeshe kupata ajira kwa kukupeleka mahali na kupewa kazi.

Haya ni mawazo mgando katika karne hii na kama bado unaota ndoto za namna hiyo basi utasubiri sana.

Sikatai kwamba tunahitaji kupewa taarifa za maeneo ambayo yana ajira na taarifa hizo tunazipata kwa kutengeneza mawasiliano na watu mbalimbali kwenye mtandao wako hususani wale ambao wako kwenye ajira.

Lakini hiyo haimaanishi kwamba ndiyo ushikwe mkono na kupewa ajira kirahisi tu, haiwezekani.

Kama ikitokea umepata kazi kwa njia hiyo, basi wewe ni mwenye bahati na mtandao wako una nguvu sana una haki ya kudeka na kujivunia kuwa na ‘God Father’ wa kukuunganisha na fursa za Ajira za namna hiyo.

Kama mwenzangu na miye ni mbula ulalo pangu pakavu, ndugu yangu komaa mwenyewe kutafuta fursa za ajira kwa kuwania kila fursa unayoiona au unayopewa taarifa na mtandao wako bila kujali unamjua nani katika taasisi hiyo.

Mkumbuke tu kwamba wanaofanikiwa ni wale wenye uthubutu wa kuchangamkia fursa pale zinapojitokeza, Watu hawa huwa na positive attitude na kujiamini hata pale wanapokatishwa tamaa kwamba haiwezekani.

Tofauti na zamani, siku hizi mitandaoni Intaneti imerahisisha sana. Kuna mitandao inayotangaza nafasi za ajira mingi sana lakini pia kampuni mengi katika touti zao kuna kipengele cha ajira ambapo humo huwekwa nafasi za kazi zinapojitokeza lakini pia nyingine zinaruhusu muombaji kujisajili na kuweka taarifa zake hata kama hakuna ajira ili zikijitokeza wanakuita kwa usaili.

Kwa mfano, zipo kampuni kubwa za kimataifa na mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO0 za kimataifa huwa zinatoa fursa za ajira popote duniani katika maeneo waliyoweka matawi iwapo zinajitokeza nafasi za kazi.

Wenzetu wa nchi jirani wamechangamkia sana fursa hizo na ndiyo maana utawakuta popote utakapokwenda hapa duniani. Lakini vijana wetu ni waoga na hawana sifa ya uthubutu.

Utakuta kijana muda wote saa 24 siku saba yuko kwenye mitandao ya Twitter, Facebook, Instagram akipiga soga lakini anashindwa kutumia muda wake kwenye mitandao ya ajira kutafuta kazi. 

Lakini hata kujifunza zaidi kile alichosomea kupitia mitandaoni ya Intaneti au kutafuta taarifa mbalimbali zinazohusiana na taaluma aliyosomea anashindwa na anajikita kwenye mijadala isiyo na tija.

Suala la kusubiri kushikwa mkono ili kupata fursa linawagusa pia wajasiriamali, nao kwa upande wao wakishaanzisha biashara  hawajiongezi kwa kupanua wigo wao wa masoko na badala yake wanategemea soko hilo hilo na hivyo wanajikuta mtaji hausogei.

Lakini watu hawa hawajui kwamba baadhi ya kampuni kuanzia mwezi wa nane hadi wa kumi na moja wanatangaza tenda mbalimbali za kununua huduma na bidhaa mbalimbali.

Ukienda kwenye kampuni haya unakuta sanduku kubwa za zabuni limeandikwa Tender Box.

Iwapo utazungumza na mtu wa mapokezi atakwambia bidhaa na huduma zinazoshindaniwa pamoja na vigezo na masharti yanayozingatiwa kwa waombaji.

Lakini ukimuuliza mjasiriamali yeyote kama huwa anachangamkia fursa hizo atakwambia hizo tenda zinatolewa kwa kujuana. Sababu ya kijinga kabisa.

Hivi ni nani aliwaambia hizi kampuni na mashirika ya kimataifa yanafanya mambo kwa kujuana? Inawezekana baadhi ya wafanyakazi wakawashika sikia watu wanaowajua na kuwadokeza kuhusu fursa zilizopo kwenye mashirika yao lakini hawana uwezo wa ku kushawishi watu hao wapate fursa hizo.

Uchambuzi wa zabuni haufanywi na mtu mmoja bali kuna kamati maalum ambayo huteuliwa tena ghafla kwa kustukizwa.

Kwa hiyo hata kama kuna mtu aliambiwa na mtu wa ndani ya shirika au taasisi kuhusu fursa za tenda muda wa kuchambua tenda Ukifika hakuna cha Mjomba.

Kwa kawaida kama akitokea mfanyakazi yeyote akionekana au akigundulika ana maslahi na miongoni mwa walioleta tenda anaondolewa kwenye kamati na huenda akapelekwa kwenye kamati ya maadili kushitakiwa na akionekana alifanya makosa ataadhibiwa na huenda akapoteza ajira.

Yees! hivyo basi kijana unatakiwa kujiamini na kuachana kabisa na misemo iliyopitwa na wakati kupata kazi ni wewe mwenyewe  namna utakavyoamua kujipambania katika maisha yako Go-go-go my friend never say Noooo always






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Shaban Kaluse

A Sales and Marketing in the hospitality Industry and also a freelance journalist, writing about love and relationships and educative articles which aims for youths, every Tuesday on Mwananchi Scoop.


Latest Post

Latest Tags