Miaka 28 imetimia tangu kifo cha Tupac Shakur

Miaka 28 imetimia tangu kifo cha Tupac Shakur

Tarehe kama ya leo mwanamuziki kutoa Marekani Tupac Shakur alifariki dunia baada ya kupigwa risasi katika mitaa ya Los Angeles nchini humo.
Ikiwa ni miaka 28 sasa imepita tangu kutokea kwa kifo hicho jina lake bado linaendelea kutajwa kutokana na makubwa aliyowahi kufanya kwenye kiwanda cha burudani.

Kutokana na utata wa kifo cha mwanamuziki huyu yapo matukio makubwa ambayo yametokea huku baadhi ya mastaa wakihusishwa katika kifo chake.

Duane “Keefe D” Davis kukamatwa na polisi
Duane ‘Keefe D’ Davis ambaye alikuwa shahidi namba moja katika mauaji ya Tupac Shakur, alikamatwa na polisi Septemba 2023 akihusishwa moja kwa moja na mauaji ya msanii huyo.

Utakumbuka kuwa Davis ambaye alikuwa rafiki wa karibu wa Tupac alihusishwa na mauaji hayo baada ya kuonekana na Tupac siku ya tukio. Hata hivyo, licha ya kuwa gerezani mpaka sasa aliwahi kuomba lakini jaji wa Mahakama ya Wilaya ya Clark, Carli Kierny alikataa kuidhinisha dhamana hiyo kutokana na kuwa na hisia mbaya na mtoaji wa dhamana hiyo ‘Wack 100’.

Aidha kesi hiyo bado inaendelea mahakamani huku ikisogezwa mbele na kuanza kusikilizwa tena Machi 17, 2024.

Diddy kuchunguzwa na familia ya Tupac
Licha ya Davis kuhusishwa katika kesi hiyo yupo mwanamuziki Diddy ambaye anadaiwa kumlipa Keef D takribani dola milioni 1 sawa na Sh 2 bilioni, kukamilisha mauaji ya Tupac.

Kutokana na tuhuma hizo zilizowahi kusambaa mitandaoni familia ya Tupac, Julai mwaka huu ilipeleka shauri mahakamani la kufanyia uchunguzi tuhuma hizo huku wakiwalipa wanasheria wakubwa nchini humo kama Alex Spiro na Christopher Clore kufuatilia madai ya Diddy kuhusika na kifo cha Tupac huku wakiamini huenda mkali huyo anafahamu kitu kuhusu kifo hicho hivyo wanataka suala hilo lichunguzwe kwa kina.

Kendrick Lamar atajwa kuvunja rekodi ya Tupac
Mbali na kuendelea kwa uchunguzi wa kumsaka aliyehusika katika mauaji hayo, kwenye upande wa burudani rapa Lamar amefanikiwa kuivunja rekodi iliyowahi kuwekwa na Tupac kufuatia na wimbo wake wa ‘Not Like Us’ kupata streams zaidi ya milioni 647.

‘Not Like Us’ ulipata mafanikio hayo na kuupiku wimbo wa 2Pac ‘Hit ‘Em Up’ kwa karibu stream milioni sita, na kuifanya ngoma ya Lamar kuwa diss track yenye stream nyingi zaidi.

Ikumbukwe kuwa Tupac alizaliwa Juni 16, 1971 na alifariki Septemba 13, 1996 akiwa na miaka 25, huku kesi ya mauaji ya kifo chake bado inaendelea mahakamani.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags