Mapenzi yalivyowaingiza mastaa wa kike kwenye kiwanda cha Video Queens

Mapenzi yalivyowaingiza mastaa wa kike kwenye kiwanda cha Video Queens

Unaweza kuutumia msemo wa "Kwenye mafanikio ya kila mwanaume nyuma yake yupo mwanamke", kutokana na baadhi ya video za nyimbo za wasanii wa kiume Bongo walizofanya wakiwa na wapenzi wao kufanya vizuri kwenye Mtandao wa YouTube.

Mbali na zile video za wasanii wa kiume zilizofanya vizuri wakiwa na warembo wengine wa kawaida, lakini walizofanya na warembo Video Queens ambao ni wapenzi wao nazo hazipo kinyonge kwani zimetazamwa na zaidi ya watu milioni. 

Hii imejidhihirisha kwa wasanii kama Harmonize ambaye mwaka mmoja uliopita kabla ya kuachana na Kajala, aliachia video ya wimbo uitwao 'Nitaubeba' huku ndani yake mrembo huyo mwenye mtoto mmoja akiwa ameipamba video hiyo.

Uwepo wa mwanadada huyo kwenye video hiyo unatajwa kama sababu ya kuipeleka mbele zaidi kinamba ambapo  hadi sasa tayari imetazamwa mara milioni 26.

Mbali na Kajala, awali wakati Harmonize anatoka akiwa mikononi mwa WCB aliwahi kuwa kwenye mahusianao na mwigizaji Irene Wolper, ambapo pia aliwahi kumtumia kama Video Queen kwenye wimbo wa 'Niambie' na hadi sasa wimbo huo uliotoka miaka saba iliyopita umetazamwa mara milioni 24. 

Rayvanny kwenye wimbo uitwao 'Wanaweweseka' uliotoka miaka mitatu iliyopita, aliweza kumchecheza Paula binti Majani kwenye video ya wimbo huo, na  hadi sasa mafanikio yake kwenye mtandao wa YouTube umetazamwa mara milioni 13. Ikumbukwe wawili hao baada ya kuachana waligeuka paka na panya na sasa Paula ni mzazi mwenzie na Marioo wakibahatika kupata mtoto mmoja wa kike aitwaye Amara.

Hata hivyo baada ya Rayvanny kutemana na Paula akarudisha majeshi kwa mzazi mwenzie Fahyma. Ndipo kupitia wimbo wa 'Forever' uliotoka mwaka mmoja uliopita Fahyma alionekana ndani ya video ya wimbo huo ambao umefikia mafanikio ya kutaamwa mara milioni kumi. 

Hakuishia hapo, miezi tisa iliyopita Fahyma akaonekana tena kwenye video ya wimbo uitwao 'Mwambieni' aliofanya Rayvanny na msanii wake Macvoice na hadi sasa wimbo huo umefikisha watazamaji milioni 5.5.

Ikumbukwe kabla ya Rayvanny kuwa kwenye mahusiano na Paula miaka sita iliyopita aliwahi kumtumia Fahyma kama video queen kwenye wimbo wake uitwa Siri aliofanya na Nikki wa Pili hadi sasa wimbo huo umetazamwa mara milioni 9.7.

Baada ya Paula kutemana na Rayvanny, akapenda boga na ua lake kwa Marioo hadi kufikia hatua ya kuonekana kwenye video ya wimbo wa mkali huyo uitwao 'Sing' uliotoka mwaka mmoja uliopita na kwenye mtandao wa YouTube umetazamwa mara milioni 2.7 hadi sasa.

Siyo hiyo tu pia Paula alikuwepo kwenye video ya wimbo wa Tomorrow na Lonely zote za Marioo

Kwenye ngoma ya Diamond aliyomshirikisha Rayvanny miaka sita iliyopita iitwayo Iyena, ilipambwa na ‘couple’ wapenzi mbalimbali wakiwemo Diamond na Zari ambapo wawili hao wamebahatika kupata watoto wawili pamoja, Tiffa na Nillan.

Mbali na warembo hao ambapo hawapo kwenye kiwanda cha muziki, wapo wasanii mwengine waliopo kwenye mahusiano wamekuwa wakishirikishana kwenye kazi zao kama afanyavyo Diamond na Zuchu, Nandy na Billnass, Aika na Nahreel pia waliwahi kufanya hivyo Diamond na Tanasha kwenye Gere ama Jux na Vanessa Mdee.

Hiyo yote inaonesha kuwa kuna wakati mahusiano yanaweza kutumika kama sehemu ya  mkakati wa kibiashara. Hivyo basi wapenzi wanaweza kuchangia katika kuongeza umaarufu wa video, kuongeza ushirikiano wa kibiashara, na kuvutia watazamaji wengi zaidi kwa sababu ya uhusiano.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Christina Lucas


Latest Post

Latest Tags