MAHUSIANO: Baadhi ya wanaume wana kichaa cha ‘kimya kimya’ cha ngono

MAHUSIANO: Baadhi ya wanaume wana kichaa cha ‘kimya kimya’ cha ngono

Naamini bila shaka wapo baadhi ya wanawake wanaweza kukiri kukutana na wanaume wenye hamu kubwa ya kushiriki tendo la kujamiiana kuliko kawaida.

Wanaweza wakawa ni wenzi wao au wanaume waliowahi kuwa na mahusiano nao kipindi cha nyuma. Kwa wale ambao bado wako kwenye mahusiano au wameolewa na wanaume wenye tatizo hili la kuwa na kiwango kikubwa cha hamu ya tendo la kujamiiana, basi wasije wakadhani kwamba wenzi wao wamelogwa, si kweli, bali hili ni tatizo la kisaikolojia.

Kitaalamu tatizo hili linafahamika kama sexual addiction. Hii ni hali ambayo huwakabili zaidi wanaume, ingawa pia inawakabili wanawake wachache. Katika hali hii ambayo inaweza kuitwa kichaa cha ngono, hutokea mwanaume kupenda tendo la kujamiiana kiasi cha kushangaza na kutisha pia. Ni kwamba, mwanaume mwenye tatizo hili anakuwa kama amepagawa na hamu kubwa ya kushiriki tendo la kujamiiana kiasi kwamba hawezi kabisa kujizuia.

Mawazo ya ngono na kushiriki jambo hilo, huitawala akili ya mhusika katika muda wake mwingi. Mawazo yake hujaa picha za ngono kiasi kwamba, huingilia hata utaratibu wa kazi zake na kumfanya pia kuvuruga uhusiano wake na mpenzi, mkewe na watu wengine wanaomzunguka.

Kwanini anavuruga uhusiano wake na mke na watu wengine?

Ni kwa sababu, kutokana na hamu yake kubwa na isiyokatika ya tendo la ndoa, hufikia mahali ambapo humtongoza yeyote anayekuwa karibu naye, iwe ni shemeji yake, mkwewe, jirani, mke wa ndugu, mke wa rafiki, mtumishi wa ndani na wengine. Hata hivyo watu wenye kichaa hiki huwa hawakubali kwamba, wana tatizo. Wanachojaribu kufanya ni kuhalalisha hizo tabia zao. Huweza hata kuwalaumu watu wengine kwa tatizo hilo.

Siyo tu kwamba, hupenda ngono kupindukia, lakini pia hufanya ngono hizo kwa njia za hatari na pia hawajali usalama wao wanapotaka kushiriki na wanawake kwenye tendo la kujamiiana. Siyo ajabu kwa mwanaume mwenye tatizo hili kwenda nyumbani kwa mwanamke anayemtaka, bila kujali kama ameolewa au hapana. Wako tayari kuhonga mamilioni ya fedha na kuacha familia zao zikifa njaa, ili mradi wawapate wanawake fulani. Kwa hiyo, mara zote wanakuwa kwenye matatizo ya kimwili na kiakili pia.

Kuna wakati watu wenye tatizo hili huweza hata kupiga simu za matusi au kutuma ujumbe mfupi wa simu ya mkononi unaoelezea mambo ya ngono kwa watu ambao wanawataka kimapenzi bila kujali mazingira. Lakini wale wanaozidiwa sana na tatizo hili, wanaweza hata kufanya mambo yenye kushangaza kuhusiana na tendo la ndoa. Kwa mfano, kuna wanaoweza kufikia hatua ya kuonesha sehemu zao za siri kwa makusudi kabisa kwa wanawake.

Tabia nyingine ambazo huambatana na tatizo hili, ni pamoja na kujichukia kwa kiwango cha juu sana, kuchukua makahaba, kuangalia sana picha za ngono, kufanya ngono zembe, yaani kufanya ngono hovyo bila kutumia kinga ya maradhi au ujauzito. Kupenda kuchungulia watu wengine wakifanya mapenzi (Kupiga chabo, kudhalilisha wanawake kijinsia (Kushikwa na mfadhaiko pale anakugusana kimwili na mwanamke, mfano kwenye vyombo vya usafiri kama daladala nk) na hata kubaka.

Kwa sababu huwa hawaridhishwi na wale wanaofanya nao mapenzi, watu wenye tatizo hili huwa hawajui kupenda, bali wanajua kufanya mapenzi tu basi. Hata hivyo, kuna wakati watu hawa hushtakiwa na dhamira na kuona aibu kutokana na vitendo vyao. Ni kama ilivyo kwa watumiaji wa dawa za kulevya, ambapo wanataka kutoka katika uraibu huo lakini wanashindwa, ingawa wanajua na kuona athari zinazowakabili.

Hata hivyo wengi kati ya watu wenye tatizo hili hawakubali kwamba, wana tatizo na ndiyo maana inakuwa vigumu sana hata kuwasaidia kuondokana nalo. Bila kukubali kwamba, ana tatizo inakuwa ni vigumu au haiwezekani kabisa kumsaidia kutoka kwenye tatizo hilo. Kuna wakati inabidi mtu apoteze kazi, ndoa ivunjike au apate matatizo ya kisheria kwa kufungwa gerezani kwa makosa ya kudhalilisha kijinsia au kubaka na wakati mwingine hata matatizo ya kiafya ndipo anapoweza kukiri kwamba, ana matatizo na hivyo kuomba msaada wa kutaka kusaidiwa.

Kama mtu mwenye tatizo hili atakuwa tayari kusaidiwa, njia kubwa inayotumika ni kwa kuanza kumsaidia kujua kinachomfanya awe kwenye tabia hiyo na kukidhibiti kitu hicho. Kwa kawaida huduma ya ushauri wa kisaikolojia ndiyo inayoweza kumsaidia mtu mwenye tatizo hilo kuondoka kwenye tabia hiyo. Pamoja na kwamba, huchukua muda mrefu hadi mtu kupona na kuacha tabia hiyo, lakini imebainika kwamba, hii ndiyo njia muafaka inayoweza kumsaidia mtu mwenye tatizo hilo kuacha tabia hiyo na kuwa mtu mpya. Kuna wakati huduma ya kitabibu inaweza kutumika kumaliza tatizo hilo pia.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Shaban Kaluse

A Sales and Marketing in the hospitality Industry and also a freelance journalist, writing about love and relationships and educative articles which aims for youths, every Tuesday on Mwananchi Scoop.


Latest Post