Kuzificha siri kwa mwenzi wako ni kujitafutia muhali

Kuzificha siri kwa mwenzi wako ni kujitafutia muhali

Hebu nikuulize wewe mwanamke. Je umewahi kumficha mumeo au mpenzi wako kitu chochote kuhusu maisha yako ya zamani au ya sasa? Je mumeo au mpenzi wako ameshawahi kukushangaza na siri ya mambo yake ya zamani?

Inawezekana jibu likawa ndiyo au hapana, lakini kuanzia leo ningependa ujifunze jambo moja kwamba ni siri gani unatakiwa kuzitoa na ni siri gani hutakiwi kuzitoa.

Usijidanganye kwamba unaweza kuficha kila siri, lakini usijiamini kwamba kwa sababu unaitwa ‘honey’ au 'sweetheart' ukitoa kila siri utaweza kunyoosha uhusiano wenu, thubutuu….!

Lengo la kuficha jambo ni kwa ajili ya kujilinda. Unaweza kudhani kwamba, kwa kusema siri zako za zamani za masuala yako ya mapenzi utaonekana shujaa utaonekana mwadilifu au utaonekana mcha Mungu.

Hapana, kuna wakati kusema kila jambo, kunakufanya ushindwe kujilinda na kumlinda mwenzi wako. Kuna mambo ambayo huna budi kuyatoa, kama siri uliyonayo inaweza kuyumbisha mustakabali wa uhusiano wenu au kuweza kuvunja ndoa yenu.

Mtaalamu wa uhusiano na mtunzi wa kitabu cha Is He Mr. Right? Mira Kirshenbaum, anasema, hata mambo ya zamani ambayo yanaweza kuleta athari katika uhusiano au maisha ya ndoa (madeni sugu, magonjwa ya kurithi, wapenzi wa zamani, tabia mbaya ambazo ulikuwa ukifanya zamani) inabidi visemwe, kutegemea tu nafasi kama vitakuja kufahamika au la.

Lakini kumbuka, kama jambo linafahamika kwa zaidi ya mtu mmoja, siyo siri, litakuja kumfikia mwenzio tu.

Kuna wakati wanandoa wanaona kama wamechelewa kutoa siri na hivyo hunyamaza na baadae siri inapofichuka watu wanaanza kuchanganyikiwa.

Lakini ukweli ni kutojua tu, pale unapokumbuka siri, ambayo una uhakika itafahamika kwa mwenzio, iseme, usisubiri. Tatizo la siri, ni kuwa huwa inaumiza sana. Kwa binadamu wengi kufuta uongo au usaliti siyo jambo rahisi.

Mtu aliyefichwa siri anajiona kwamba alisalitiwa, kwa hiyo hujenga chuki kubwa. Hata kama unaona siri yako ni kuhusu jambo dogo kwako, tafadhali usimfiche mwenzio.

Kama ukweli wa jambo hilo utakuja kujulikana baadae, madhara yanaweza kuwa mabaya zaidi kuliko kama ungekuwa umemwambia mapema. Sio kwamba mwenzi wako anahitaji kupata habari ili mshirikiane kutatatua jambo lililo mbele yenu, lakini pia anahitaji kwa ajili ya kujua kama unamwamini.

Ipo kanuni moja kuhusu mapenzi inasema unavyozidi kutotaka kuitoa siri ndivyo unavyoiombea ijitokeze ghafla na kuanikwa hadharani.

Vipi kuhusu mpenzi wako wa zamani kwamba anaweza akajitokeza ghafla ikajulikana kwa mumeo? Kama unahisi kwamba mwenzi wako anaweza kuja kupata habari za mpenzi huyo wa zamani, basi hakikisha kwamba unamweleza kabla hajatambua. Kujisafisha na wapenzi wako wa zamani ni jambo zuri.

Bali jaribu kuwa mwangalifu, si lazima katika maelezo yako ukaanza kumsimulia mwenzio hata upuuzi mliokuwa mkifanya wakati wa mapenzi yenu.

Ni wajinga tu ndio wanaofanya hivyo. Wenye hekima husema tu ukweli kwamba, waliwahi kuwa na uhusiano na huyu au yule na fulani na fulani.

Hata kama ni kumi, wataje, ili mwenzio aamue mwenyewe, usijidanganye kwamba, hatakuja kujua. Watangulie wambea mapema kabisaa, ili wakija kumnong’oneza awaambie,

‘ninajua’

Wapo wanawake wengine huyumbisha uhusiano na wenza wao au ndoa zao kwa kufukunyua mambo madogo madogo. Si vyema sana kuleta udadisi kwenye mambo madogo madogo ambayo hata hayana maana wakati mwingine.

Usimsumbue mwenzio kutokana na gharama ya simu yake ya mkononi au kamera yake, hasa kama na wewe hutaki akuulize kuhusu bei ya mkoba au kidani chako.

Vipi, wewe unafichaga siri zako au la na kwanini? Tupa comment hapo chini.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Shaban Kaluse

A Sales and Marketing in the hospitality Industry and also a freelance journalist, writing about love and relationships and educative articles which aims for youths, every Tuesday on Mwananchi Scoop.


Latest Post

Latest Tags