Jinsi ya kukabiliana na mazingira magumu ukiwa kazini

Jinsi ya kukabiliana na mazingira magumu ukiwa kazini

Ooyeeah! Leo katika kazi, ujuzi na maarifa leo  tunakuletea mbinu ambazo zitakusaidia kukabiliana na kuhimili  mazingira magumu kazini ili yasiweze kukupa stress.

Sio kitu cha ajabu kuchukia kazi yako. Lakini, mara nyingine chuki yako ya kazi haisababishwa na kazi yenyewe, bali watu unaofanya nao kazi na mazingira kiujumla.

 Pia, kuacha kazi papo hapo sio fursa ambayo kila mtu anayo kwa sababu ya gharama kubwa za maisha Tanzania na ushindani katika soko la ajira.

Hivyo unaweza kuta umenasa kwenye kazi usiyoipenda kwa muda mrefu. Sasa, kama una bosi anaye kuonea au wafanyakazi wenzako ni wajeuri, unawezaje kuhimili mazingira magumu ya kazi?

  1. Weka rekodi ya kila kitu

Kama unafanya kazi na bosi au mfanyakazi mwenza msumbufu, hakikisha mawasiliano yote kati yenu yanafanyika kwa njia ya maandishi kama barua pepe. Hakikisha unatumia lugha safi na inayoeleweka kwenye nyaraka zote za kitaalamu. Hii itakusaidia hasa, mfano wakati mfanyakazi mwenzako anakutongoza kimapenzi.

2.Achana na umbea

Usiongeze ukubwa wa matatizo kwa kusambaza habari kuhusu bosi wako au mfanyakazi mwingine ofisini, hata kama wana makosa. Kwa sababu ukishaanza kusambaza habari, na wewe unakua ni sehemu ya tatizo. Pia, si jambo zuri kuchochea wafanyakazi wenzako kuchagua pande za kushabikia, kwa sababu mwishoni inabidi wote mfanye kazi pamoja.

  1. Omba ushauri kutoka kwa Afisa Rasilimali Watu (HR).

Kama tatizo limekuwa kubwa kiasi kwamba mahala pa kazi si sehemu salama basi wasiliana na HR. Usiogope kutoa taarifa hata kama tatizo linamhusisha bosi wako. Ni wajibu wa HR kuhakikisha kuwa mahala pa kazi ni sehemu salama kwako. Pia, hii ni namna mojawapo ya kuweka rekodi ya tatizo kwa ajili ya kujilinda kama itatokea kesi ya kisheria

  1. Zungumza na mhusika

Inawezekana tatizo lililopo ni sababu ya kuto kuelewana tu. Hivyo ni bora kujaribu kukaa chini na kuzungumza na mhusika uongee upande wako na usikilize upande wake. Hii haimaanishi umshambulie na kumpa mzigo wote wa tatizo yeye, kwani hii itamfanya atake kujilinda. Badala yake, tumia lugha fasaha kama, “Ulivyosema hivi, mimi nilielewa hivi.

  1. Zingatia malengo yako

Mahala pa kazi pagumu panaweza kukufanya usahau kwanini ulikubali kazi hapo mwanzoni. Kama unapenda kazi unayoifanya lakini unakerwa na watu unaofanya nao kazi, elekeza nguvu zako kwenye kufikia malengo yako ya kikazi. Jitihada zako zitakuwezesha kupita vikwazo vyote.

  1. Tafuta kitu cha ziada cha kufanya

Wakati mwingine kuwa na jambo la kufanya nje ya kazi unalolipenda kunaweza kuongeza uwiano kati ya maisha yako binafsi na maisha yako ya kazi, hivyo kukuwezesha kuendelea na kazi. Pia inaweza kusaidia kuondoa fikra zako kwenye matatizo unayopata kazini.

  1. Tafuta mtu wa kuongea nae nje ya kazi

Ni vizuri kuzungumza kuhusu matatizo yako na mtu anaekujali, ambaye anaweza kukupa ushauri mzuri. Lakini, jitahidi mtu huyo awe ni wa nje ya kazini kwako ili kuepuka umbea na maneno maneno yasiyo ya msingi

  1. Acha matatizo yako kazini

Usisome barua pepe zozote za kazini nje ya muda wa kazi ili kupunguza mawazo kuhusu matatizo yako ya kazini.

9.Tumia muda wako kutafakari

Kama unapata matatizo mara kwa mara na watu tofauti kazini, inabidi ujitathmini kama wewe ndio mwenye tatizo. Angalia matukio ambayo yalisababisha mgogoro, na wewe ulihusika vipi. Kama huoni makosa yako, jaribu kushirkisha mtu mwengine usikie mtazamo wake

  1. Tengeneza mkakati wa kuondoka

Kama yote haya yameshindikana na huoni njia ya kutatua matatizo yako basi ni bora upange mkakati wa kuondoka. Jipangie muda wa kutafuta kazi na kuacha kazi uliyonayo, Pia unaweza kuhifadhi sehemu ya kipato chako kikusaidie pale utakapoacha kazi kabla hujapata nyingine. Kawaida ukishapanga mkakati wa kuondoka utapata ahueni sababu unajua unaondoka lini, hivyo unajua mwisho wa matatizo yako.

Unapofanya kazi na watu wasumbufu au sehemu yenye sera zinazobana, inatakiwa ujue ni nini kipo kwenye uwezo wako kubadilisha au kudhibiti. Kwa mfano unaweza kumshirikisha HR kwenye migogoro na kuweka rekodi ili ikitokea kesi ya kisheria kuwe na ushahidi. Unaweza kutengeneza taswira yako kwa kutoa ushirikiano mzuri kwa wafanyakazi wenzako. Unaweza kujizuia jazba pale unapokabiliana na matatizo. Lakini hauwezi kudhibiti tabia za wafanyakazi wenzako. Huwezi kuwafanya wawe watu wakarimu, hivyo usijaribu kufanya hivyo, kumbuka sababu yako ya kuwa kazini.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags