Kwa sasa si jambo la kushangaza tena nyimbo za wasanii wa Afrika kupenya kwenye chati maarufu duniani za Billboard na kuwafanya mastaa hao watambulike zaidi. Wapo waliofanya vizuri kwa mwaka 2024 kwenye chati hizo. Lakini kwa sasa kumekuwa na mijadala mbalimbali ikihoji nani atakayetikisa kwa mwaka 2025.
Mwaka 2021, msanii wa Nigeria CKay alijifungulia njia kupitia wimbo wake wa ‘Love Nwantiti’ alioutoa 2019 ambapo wimbo huo ulianza kuorodheshwa kwenye Billboard Hot 100, huku ukikusanya mabilioni ya wasikilizaji katika mitandao mingine ya kusikiliza na kuuza muziki.
2022, mwanamuziki Rema kupitia wimbo wake ‘Calm Down’ alifanikiwa kuiteka dunia kupitia ngoma hiyo huku akifanikiwa kukaa katika chati za Billboard kwa muda mrefu zaidi.
Kutokana na ngoma hiyo kuwa kali mwanamuziki wa Marekani Selena Gomez akishirikiana na Rema waliifanyia remix jambo lililopelekea wimbo huo kupata mauzo na kusikilizwa zaidi huku ukikaa kwa wiki 51 mfululizo kwenye US Billboard Afrobeats Chart.
Mbali na hao akiwa na umri wa miaka 21 ilitosha Tyla kuonesha ukubwa wake, ambapo mwaka 2023 kupitia wimbo wake 'water'aliiwakilisha Afrika katika chati hizo na kuufanya ufike hadi nafasi ya kwanza kwenye Billboard.
Kwa mwaka 2024, msanii huyo aliendelea kuiteka chati hiyo kupitia album aliyoipa jina lake ‘TYLA’ ikibeba ngoma kama Truth or Dare, Butterflies, Water remix akimshirikisha Travis Scott na nyinginezo ambazo pia zimepenya katika chati hizo na kupata wasikilizaji wengi zaidi.
Ukiachana na Tyla kwa mwaka 2024 naye mwanamuziki kutoka Tanzania Diamond alifanikiwa kupenya katika chati hizo kupitia wimbo wake ‘Komasava Remix’ ukiwa wimbo wa kwanza kutoka Tanzania kufikia mafanikio hayo.
Hayo ni mafanikio ya baadhi ya wasanii Afrika kwenye chati hizo. Swali ni nani ataibeba Afrika mwaka 2025.
![Yupi Ataiwakilisha Afrika Chati Za Billboard 2025](https://mwananchiscoop.co.tz/public/uploads/2025/02/05/frceecc8a8da1d6f2c4579798853537968ab8b9c98.jpg)
Leave a Reply