Moja ya kitu ambacho kimekuwa kigumu kukipata kwa rapa wengi wa sasa ni kuchana mitindo huru 'Freestyle'. Hii ni mistari ambayo inashushwa moja kwa moja bila kuandikwa, inaweza kuchanwa juu ya biti au bila biti.
Kontawa ni rapa ambaye anafahamika zaidi kwa uwezo wake wa kuchana na kuimba kama vile ambavyo anasema mwenyewe anafanya 'Melodic rap'. Kitu ambacho wanafanya hata wasanii wakubwa duniani kama, Drake, Post Malone, Lil Durk, Gunna, Lil Wayne, Travis Scott, Kid Cudi na wengine wengi.
Ukifuatilia kwa umakini katika baadhi ya mahojiano aliyoyafanya Kontawa na kupewa nafasi ya kuchana utagundua ana uwezo mkubwa wa kufanya kitu hicho ambacho rapa wengi wa sasa imekuwa mtihani kwao.
Licha ya watu kuanza kutambua uwezo wake mwingine katika muziki. Kwa mujibu wake anakwambia kabla ya kuanza kuandika nyimbo alikuwa anafanya freestyle na ndio maana kwake sio kazi.
Ieleweke, sio kwamba tasnia ya muziki haina wasanii wakali wa kufree style kumshinda Kontawa. Lakini kwa sasa naweza kusema yeye ndio msanii wa rapu wa kizazi chake ambaye anafanya vizuri kwenye nyimbo za kuandika, pia anauwezo wa kufree style.
Kontawa ananikumbusha enzi za wasanii wa hiphop nchini ambao wametangulia mbele za haki kama Godzilla na Ngwea. Ambao walikuwa moja ya wakali wa free style na kuandika nyimbo katika kipindi chao walichohudumu kwenye muziki wa Bongo Fleva.
Wasanii wengine wa kizazi hiki ambao ni wakali wa free style ni pamoja na Toxic 'Fuvu', Wizzy MP, Kado Kitengo na wengine wengi.

Leave a Reply