Mwigizaji anayetamba katika tamthilia ya ‘Kombolela’ Happy Swebe maarufu kama ‘Tabu wa Kombolela’ amefunguka ugumu anaopitia katika uhusika wake wa bubu.
Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu Tabu ameeleza kuwa changamoto anayopitia katika uhusika huo ni sauti kukauka.
“Ugumu wa kuigiza kama bubu upo kwa sababu nawakilisha uhusika wa mtu ambaye hazungumzi na mimi nazungumza. Ugumu unakuja kuna namna natakiwa kutoa sauti ya tofuti nikiwa na hasira, nalia au nikiwa napiga kelele kuna sauti natakiwa kuitengeneza ambayo kila mtu atajua kabisa kwamba yule ni bubu bila ya kuzungumza chochote.
“Kwa hiyo ninavyotumia hiyo sauti kuna wakati sauti yangu inakauka kabisa.Pia nimekuwa naulizwa sana hili swali, nataka kuwaambia mashabiki kuwa mimi sio bubu ule ni uhusika tuu,” amesema Tabu
Aidha ameongezea kwa kueleza “Uhusika wangu bora tangu nianze kuigiza mpaka sasa ni huu wa bubu. Yaani naipenda sana hii ‘karakta’ na naikubali kwa sababu ni uhusika ambao watu wengi wamenifahamu kupitia Tabu. Ni uhusika ambao wa tofauti kwangu, kwanza ni mgumu ambao unanipa changamoto ya kujifunza vitu vingi lazima nisome nijue bubu wanatumia ishara gani, naukubali sana,” amesema
Akizungumza kuhusu tamthilia ya Kombolela kumpatia michongo na umaarufu Tabu ameeleza,
“Kombolela kwa upande wangu imenipa ‘Koneksheni’, imenipa umaarufu watu wengi wananijua kupitia tamthilia hiyo. Imekuwa sababu kubwa ya mimi kutafutwa katika kazi, matangazo yaani naweza kusema Kombolela imenifungulia njia,” amesema Tabu
Historia ya uigizaji
“Historia yangu ilianzia Mkoani Mbeya katika kijiji cha Tukuyu nilianza kipindi nasoma mwaka 2015 nilitoka Mbeya kuja Dar es Salaam kwa ajili ya sanaa. Nilivyofika nilijiunga makundi ya uigizaji, nilifanya mazoezi kwenye makundi mengi sana lakini sikufanikiwa kuchaguliwa kuigiza sehemu yoyote.
“2016 nilipata nafasi ya kushiriki tamthilia ya ‘Maneno ya Kuambiwa’ iliyoandaliwa na Kitale, baada ya kumaliza, sikuendelea na sanaa niliacha kutokana na sababu zilizokuwa nje ya uwezo wangu. Kipindi kile niliamua kurudi tena mkoani. 2021 nilirudi tena Dar kwa ajili ya kupambania ndoto zangu za uigizaji,”amesema

Leave a Reply