Baada mfanyabishara Kim Kardashian kutoa ushahidi katika mahakama jijini Paris kuhusiana tukio la kuvamiwa na majambazi kwenye moja ya hoteli nchini Ufaransa, hatimaye Kim amezungumza kwa mara ya kwanza huku akiwapongeza majaji kwa kutenda haki.
“Uhalifu huu ulikuwa tukio la kutisha zaidi maishani mwangu, na umeacha athari ya kudumu kwangu na familia yangu. Ingawa sitasahau kilichotokea, naamini katika nguvu ya ukuaji na kuwajibika, na ninaomba uponyaji kwa wote. Nawapongeza sana majaji kwa kutenda haki,” amesema Kim
Aidha timu yake ya wanasheria ikiongozwa na Michael Rhodes, Léonor Hennerick, na Jonathan Mattout imetoa pongezi kwa mfanyabiashara huyo kwa ujasiri wake mwanzo mpaka mwisho wa kesi.
“Ameonyesha ujasiri mkubwa, si tu katika kukabiliana na watekaji wake bali pia katika kuendelea kutetea haki. Huu ni wakati muhimu wa kupata hitimisho kwake.”
Ikumbukwe, Jumanne Mei 13, 2025 Kim alitoa ushahidi mahakamani akieleza kuwa alidhani angenyanyaswa kimwili na kuuawa baada ya kuvamiwa na majamabazi akiwa Hotelini wakati wa wiki ya mitindo 'Paris Fashion Week' mwaka 2016.
Akizungumza mahakamani hapo wakati wa kutoa ushahidi Kim amesema katika tukio hilo alivamiwa na watu 10 na kuibiwa vito vyenye thamani zaidi ya dola 9 milioni sawa na sh 26 bilioni.
Kesi hiyo ilimalizika mapema jana Mei 23,2025 katika mahakama jijini Paris ikiwahukumu wanaume wanne waliopatikana na hatia kuhusiana na tukio hilo la mwaka 2016. Wanaume hao ni pamoja na Aomar Aït Khedache (69) kiongozi wa genge aliyehukumiwa miaka 3, Yunice Abbas (72) atatumikia miaka 2, Harminy Aït Khedache, mwaka mmoja huku wawili wakiachiwa huru ambao ni Didier Dubreucq na Marc-Alexandre Boyer.

Leave a Reply