Mfanyabiashara maarufu Marekani, Kim Kardashian amehitimu rasmi masomo yake ya sheria katika levo ya ‘Law Office Study Program (LOSP)’ levo ambayo ni njia mbadala ya kusomea sheria kwa kufanya mafunzo ya vitendo chini ya usimamizi wa wakili badala ya kuhudhuria chuo kikuu cha sheria.
Kim alisherehekea mafanikio yake kwa hafla fupi iliyoandaliwa nyumbani kwake ikihudhuriwa na familia, marafiki na washauri wake huku watoto wake wakivalia mavazi ya kisheria kama heshima ya mafanikio ya mama yao na kumbukumbu ya babu yao marehemu, Robert Kardashian Sr, ambaye alikuwa wakili maarufu.
Mfanyabiashara huyo alianza safari yake ya kujifunza sheria mwaka 2018 kwa kufanya mafunzo ya vitendo katika kampuni ya sheria iliyoko San Francisco. Ingawa masomo hayo kwa kawaida huchukua miaka minne, kwa upande wa Kim amesoma kwa miaka sita kutokana na changamoto za janga la COVID-19 na majukumu yake mengine ya kifamilia na kibiashara.
Kwa mujibu wa tovuti ya ‘People’ baada ya kuhitimu, Kim sasa anajiandaa kwa mtihani wa mwisho wa sheria wa California (bar exam) ili kupata leseni rasmi ya uwakili. Ameonyesha dhamira ya kuendeleza kazi ya baba yake na kuleta mabadiliko katika mfumo wa haki ya jinai.
Kwa sasa, Kim pia anajiandaa kuigiza kama wakili katika mfululizo mpya wa Ryan Murphy uitwao All’s Fair, unaotarajiwa kuonyeshwa kwenye Hulu msimu wa vuli wa 2025

Leave a Reply