Waandaaji Miss Tanzania Wakata Rufaa Kupinga Uamuzi Wa Basata

Waandaaji Miss Tanzania Wakata Rufaa Kupinga Uamuzi Wa Basata

Kampuni inayojihusisha na kuandaa mashindano ya Miss Tanzania, 'The Look' imekata rufaa kupinga uamuzi uliotolewa na Baraza la Sanaa la Taifa 'Basata' wa kufutiwa kibali cha kuendesha mashindao hayo.

Taarifa hiyo imetolewa leo Julai 9,2025 na kampuni ya The Look ikieleza kuwa uamuzi huo haukuwa wa haki hivyo rufaa hiyo itatenda haki kwa pande zote mbili.

“Wamiliki na waandaaji wa mashindano ya urembo ya Miss Tanzania, kupitia kampuni ya The Look Company Limited imekata rufaa kwa mheshimiwa Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, kufuatia sintofahamu ya kuondolewa sifa ya kuandaa mashindano ya urembo ya Miss Tanzania.

"Tarehe 25 June 2025 uongozi wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) kupitia ukurasa wake wa Instagram ulitoa tangazo kwa wananchi kujulisha ya kwamba Kampuni ya The Look, imeondolewa sifa ya kuandaa mashindano ya urembo ya Miss Tanzania, kutokana na kukiuka baadhi ya kanuni za baraza hilo,” imeeleza taarifa hiyo

Aidha imeendelea kwa kueleza “Baraza lilitoa muda wa siku 21 kwa Uongozi wa Kampuni ya The Look kukata rufaa kwa Waziri mwenye dhamana ya kusimamia tasnia hiyo. Uongozi wa Kampuni ya The Look umekata Rufaa kupinga uamuzi huo, tukiamini kwamba Mheshimiwa Waziri pamoja na uongozi mzima wa Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo utatenda haki na kuchukua hatua stahiki katika maamuzi yake kwa maslahi ya pande zote mbili na taifa kwa ujumla,”

Utakumbuka Juni 25,2025 Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) liliifutia kibali kampuni hiyo kuendesha Miss Tanzania likieleza kuwa uamuzi huo umetolewa baada ya kampuni hiyo kushindwa kutekeleza maagizo halali ya Baraza licha ya kupewa maelekezo kwa nyakati tofauti kupitia barua yenye kumbukumbu namba AE/90/90/03/16 ya Aprili 15, 2025, na AE.90/90/03/19 ya Mei 09, 2025.

“Kushindwa kuhuisha kibali cha kufanya kazi za sanaa kwa zaidi ya miezi sita bila sababu ya msingi, kinyume na Kanuni ya 39(g) ya Kanuni za BASATA za mwaka 2018. Kukaidi agizo la Baraza kwa kutowasilisha nyaraka muhimu kama nakala ya cheti/leseni ya kushiriki shindano la Dunia, kinyume na Kanuni za 39(f), 37(2)(a) na 36(2).

"Kushindwa kuandaa shindano la Miss Tanzania kwa mwaka 2023/2024 na kutokuwasilisha mwakilishi wa Tanzania katika mashindano ya dunia kwa mwaka 2024/2025, bila kutoa sababu za msingi, jambo linalokiuka Kanuni ya 39(i). Kwa mujibu wa Kanuni ya 40(2) ya Kanuni za BASATA za mwaka 2018, kampuni hiyo imeondolewa sifa ya kuendelea na shughuli hiyo,”ilieleza taarifa hiyo

Hata hivyo iliendelea kwa kuweka wazi kuwa “Kampuni ya The Look Company Limited inayo haki ya kukata rufaa kwa Waziri mwenye dhamana ndani ya siku 21 tangu kupokea taarifa hii. BASATA linaendelea kusimamia kwa ukamilifu utekelezaji wa sheria, kanuni na taratibu katika tasnia ya sanaa ili kulinda heshima na ufanisi wa mashindano ya kitaifa kama Miss Tanzania,”






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags